Kocha Yanga aishika pabaya FAF

KOCHA wa Yanga, Mreno Pedro Goncalves inadaiwa anataka kulipeleka Shirikisho la Soka la Angola (FAF) katika Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), kwa kile kinachodaiwa bado linamtambua ni mkufunzi kimkataba, licha ya kuondoka.

Taarifa kutoka Angola zinadai FAF, bado linamchukulia Pedro kama kocha mkuu wa timu hiyo ya taifa, huku baadhi ya masharti muhimu yanayohusu masuala ya kimkataba wake yakidaiwa kutotekelezwa tangu alipoondoka.

Vyanzo mbalimbali vinaeleza Pedro hakuwa na nia ya kulifungulia kesi shirikisho hilo kutokana na uhusiano mzuri tangu alipokuwa anafanya nalo kazi, ingawa kutotekelezwa kwa makubaliano ndio sababu inayochangia.

Hata hivyo, inadaiwa viongozi hao wa FAF wanataka kufanya mazungumzo ya haraka na ya amani na Pedro kabla ya kocha huyo hajafikia uamuzi wa mwisho wa kwenda Fifa, jambo ambalo linaweza kuwaingiza matatani na kumlipa kiasi kikubwa cha fedha.

Pedro alijiunga na Yanga Oktoba 25, 2025, kwa ajili ya kukiongoza kikosi hicho kwa msimu huu wa 2025-2026, ikiwa ni muda mfupi tangu kikosi hicho kikate tiketi ya kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2025-2026.

Yanga ilimtambulisha Pedro ikiwa ni muda mfupi tu tangu ifuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya timu hiyo kuibuka na ushindi wa mabao 2-0, dhidi ya Silver Strikers kutoka Malawi na kuiondosha kwa jumla ya mabao 2-1.

Pedro alijiunga na Yanga akiwa na rekodi nzuri pia ya kuifikisha timu ya Taifa ya Angola katika hatua ya robo fainali ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), iliyofanyika mwaka 2023 na kushuhudia wenyeji, Ivory Coast ikitwaa ubingwa huo.

Mbali na hilo, Pedro aliiongoza Angola katika Fainali za Kombe la Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa Ligi ya Ndani (CHAN), iliyofanyika mwaka 2024 katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda, ambapo timu hiyo iliishia hatua ya makundi.

Pedro alihudumu kama muibuaji wa vipaji katika Klabu ya Sporting CP nchini Ureno, kisha kituo cha kulelea vipaji cha timu hiyo kati ya 2000 hadi 2015, huku kwa mara ya kwanza Afrika aliwafundisha vijana wa Primeiro de Agosto ya Angola mwaka 2015 hadi 2018.

Kocha huyo aliifundisha klabu hiyo na ile ya vijana chini ya miaka 20 hadi 2019, kisha timu ya Angola ya wakubwa, ambapo alikifundisha kikosi hicho hadi mwaka 2025 na kuachana nacho na kujiunga na Yanga akichukua nafasi ya Romain Folz.