LICHA ya kiwango bora kinachoonyeshwa na mshambuliaji nyota wa Fountain Gate, Mnigeria Chukwunonye Obasi, lakini kocha mkuu wa timu hiyo, Mohamed Ismail ‘Laizer’ amesema kutomchezesha dakika nyingi ni kutokana na sababu mbalimbali za kimsingi.
Akizungumza na Mwanaspoti, Laizer amesema kutokana na ufinyu wa wachezaji wengi kikosini humo baada ya kufungiwa timu hiyo kutosajili, inamlazimu kuweka mikakati mizuri ya kiufundi, ambayo itamsaidia kwenye mabadiliko wakati wakizidiwa.
“Sisi kama benchi la ufundi tunaangalia upungufu mkubwa wa mpinzani wetu na maeneo ambayo tunaweza tukawashinda haraka, ni kweli, Obasi anaonyesha kiwango kizuri, ila yeye tunamtumia kwa ajili ya kumaliza mechi uwanjani,” amesema Laizer.
Laizer amesema wakati wa kupanga kikosi cha kwanza, Obasi huwa mara nyingi anapenda kumtumia kipindi cha pili, ambacho anaamini inakuwa ni mchezaji anayesababisha mabadiliko makubwa ya kiuchezaji, jambo ambalo linaongeza faida kwa wenzake.
“Mechi za hivi karibuni tumekuwa tukimuanzisha benchi kwa sababu tunapozidiwa maana yake tunahitaji mchezaji anayeweza kubadilisha mchezo na kuongeza ufanisi mkubwa katika eneo la ushambuliaji, bahati nzuri mabadiliko yake yanaleta tija,” amesema.
Nyota huyo aliyejiunga na Fountain Gate, Julai 1, 2025, baada ya kuachana na FK Usti nad Labem ya Jamhuri ya Czech, ameifungia timu hiyo mabao mawili ya Ligi Kuu Bara msimu huu, akiwa sawa na mshambuliaji mwenzake, Sadick Ramadhan.
Mshambuliaji huyo aliyezaliwa, Julai 20, 2005, mbali na kuichezea FK Usti nad Labem ya Jamhuri ya Czech, pia amewahi kucheza City FC Abuja ya kwao Nigeria, akiwa muhimili mkubwa katika kikosi cha Fountain Gate kutokana na uchezaji wake.