MAADILI YA RAMADHAN YAHIMIZWA KUDUMISHWA MBEYA

Na Mwandishi Wetu, Mbeya

MKUU wa Wilaya ya Mbeya, Solomon Itunda, amewahimiza viongozi wa dini ya Kiislamu kuendelea kusimamia na kuimarisha maadili kwa waumini hata baada ya kumalizika kwa mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Itunda ametoa wito huo wakati wa hafla ya Iftari iliyoandaliwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Erica Yegella, iliyolenga kuimarisha mshikamano miongoni mwa waumini, watumishi wa umma na wadau wa maendeleo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Itunda amesema maadili yanayojengwa wakati wa Ramadhan yanapaswa kudumishwa katika maisha ya kila siku ili kulinda amani na utulivu wa nchi.

“Niwaombe viongozi wa dini kuendelea kuhamasisha waumini kutenda mema hata baada ya Ramadhan kupita. Kama viongozi wa umma, tunalo jukumu la kuendeleza uadilifu na kuwahudumia wananchi kwa haki,” amesema Itunda.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa amani akieleza kuwa ndiyo nguzo inayowezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ukiwemo upanuzi wa barabara kutoka Igawilo hadi Tunduma unaolenga kuimarisha miundombinu ya usafirishaji na biashara.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Erica Yegella, amesema hafla hiyo imekuwa sehemu ya utamaduni wa Halmashauri hiyo kuwakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini na wafanyabiashara ili kuimarisha ushirikiano katika kuleta maendeleo ya wilaya.

Hii ni mara ya pili kwa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya kuandaa Iftari kwa ajili ya watumishi na wananchi, hatua inayotajwa kusaidia kupunguza mwanya kati ya watendaji wa serikali na jamii wanayoihudumia.