Lindi. Sauti za wanafunzi zikichanganyika na vicheko vya wananchi zilisikika katika viunga vya Shule ya Msingi Msinjahili, wakati mikono ya walimu, viongozi na wadau wa mazingira ikipanda miche ya miti kwa matumaini ya kulinda mazingira ya kesho.
Katika kuelekea maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani yanayotarajiwa kufanyika kitaifa mkoani Lindi, jumla ya miche 1,500 ya miti ya matunda, mbao na kivuli imepandwa katika shule hiyo ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kuhamasisha utunzaji wa mazingira.
Akizungumza baada ya shughuli ya upandaji miti leo Jumamosi Machi 14, 2026, Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Victoria Mwanziva amewahimiza wananchi, wanafunzi na taasisi mbalimbali kushiriki kikamilifu katika juhudi za kupanda na kutunza miti ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Mwanziva amesema miti ina mchango mkubwa katika kulinda mazingira, kuboresha hali ya hewa na kuleta manufaa mbalimbali kwa jamii ikiwemo kutoa matunda, kivuli na malighafi.
“Hapa Shule ya Msingi Msinjahili leo tumepanda miche 1,500. Niwaombe wananchi wa Manispaa ya Lindi kila mmoja awe na jukumu la kupanda na kuitunza miti ili kuhakikisha mazingira yanabaki salama kwa kizazi cha sasa na kijacho,” amesema Mwanziva.
Mkuu wa Wilaya ya Lindi Victoria Mwanziva akipanda mti wa matunda katika shule ya msingi Msinjahili leo, Jumamosi Machi 14, 2026. Picha na Bahati Mwatesa
Kwa upande wake, Saimoni Kipereja kutoka Idara ya Misitu na Nyuki ya Wizara ya Maliasili na Utalii, amesema Serikali inaendelea kuhamasisha upandaji miti nchini kama sehemu ya mkakati wa kuongeza uoto wa asili na kukabiliana na uharibifu wa mazingira.
Amesema maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani yanatarajiwa kuwakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa Serikali, taasisi, wanafunzi na wananchi kwa lengo la kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa upandaji miti na uhifadhi wa misitu.
Naye Mhifadhi wa Wilaya ya Lindi kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Gaspar Vicent amesema taasisi hiyo imekuwa ikizalisha zaidi ya miche 200,000 ya miti kila mwaka ambayo hugawiwa kwa taasisi mbalimbali na wananchi kwa ajili ya kupandwa katika maeneo tofauti.
Vicent amesema juhudi hizo zinalenga kuongeza kasi ya upandaji miti na kurejesha uoto wa asili katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Shughuli hiyo ya upandaji miti limehudhuriwa na viongozi wa Serikali, walimu, wanafunzi pamoja na wadau wa mazingira.
