Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema jeshi la nchi hiyo limefanya mashambulizi ya anga dhidi ya vituo vya kijeshi katika Kharg Island nchini Iran, akionya kuwa miundombinu muhimu ya mafuta katika eneo hilo inaweza kuwa shabaha inayofuata iwapo Iran itaendelea kuzuia meli kupita kwa uhuru katika Strait of Hormuz.
Kwa upande wake, Iran imetishia kuharibu kabisa miundombinu ya mafuta inayohusishwa na Marekani katika ukanda wa Ghuba iwapo vituo vya mafuta kwenye Kisiwa cha Kharg vitashambuliwa.
Kauli hiyo imekuja wakati vita kati ya United States, Israel na Iran vikiingia wiki ya tatu, huku mvutano huo ukichochea kupanda kwa kasi kwa bei ya mafuta duniani.

Kisiwa cha Kharg ndicho kitovu kikuu cha usafirishaji wa mafuta ghafi ya Iran kwenda nje ya nchi, kikihusika na zaidi ya asilimia 90 ya mauzo yote ya mafuta ya taifa hilo. Tangu kuanza kwa mapigano hayo, bei ya mafuta ghafi duniani imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 40 kutokana na hofu ya kuvurugika kwa usambazaji wa nishati duniani.
Trump amesema vikosi vya Marekani viliharibu kikamilifu malengo yote ya kijeshi kwenye kisiwa hicho. Hata hivyo, alieleza kuwa kwa sasa ameacha kushambulia miundombinu ya mafuta ya Iran, lakini akaonya kuwa anaweza kubadili uamuzi huo iwapo Iran au upande mwingine wowote utajaribu kuzuia usafiri salama wa meli katika Mlango wa Hormuz.

Wakati huo huo, vyombo vya habari vya Iran vimeripoti kuwa zaidi ya milipuko 15 ilisikika katika Kisiwa cha Kharg wakati wa mashambulizi hayo, yakilenga mifumo ya ulinzi wa anga, kambi ya wanamaji na miundombinu ya uwanja wa ndege.
Aidha, taarifa zimeeleza kuwa wanajeshi zaidi wa Marekani wapatao 2,500 pamoja na meli ya kijeshi aina ya USS Tripoli (LHA-7) wanapelekwa Mashariki ya Kati, huku Wizara ya Afya ya Iran ikisema watu wasiopungua 1,444 wameuawa na zaidi ya 18,500 kujeruhiwa tangu mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran yalipoanza Februari 28 mwaka huu.