MBUNGE LUTANDULA AWASHIKA MKONO WAISLAMU KWA IFUTARI BUSERESERE BWANGA

……

CHATO

MBUNGE wa Jimbo la Chato Kusini, Pascal Lukas Lutandula, ameungana na waumini wa dini ya Kiislamu kwa kuwapatia sadaka ya Ifutari, ikiwa ni ishara ya upendo, amani na ushirikiano kwa makundi yote katika Jimbo hilo.

Akikabidhi sadaka hiyo kwa niaba ya Mbunge Lutandula, Daud Makashi, amevitaja vitu vilivyokabidhiwa kuwa ni Mchele kg 300, Mafuta ya kupikia lita 60, Sukari kg 75, Tende box 3, pamoja na maji ya kunywa katoni 60.

Hatua hiyo imelenga kuongeza tabasamu kwa waumini wa dini ya Kiislamu katika mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan, ambapo itawasaidia baadhi ya waislamu kupata futari.

Amesema baadhi ya misikiti iliyoguswa na huduma hiyo ni pamoja na Msikiti wa Bakwata kata ya Buseresere, Bwanga na Nyakayondwa katika Jimbo la Chato kusini.

Kitendo cha Mbunge Lutandula kuguswa na funga kisha kutoa sadaka hiyo, imeakisi kauli ya mwanamuziki maarufu na mwanzilishi wa miondoko ya Raggae duniani, Robert Nesta Marley kuwa “Rafiki wa kweli ni kama nyota, utamtambua wakati wa giza litakapokuwa limekuzunguka”.

Akipokea zawadi hiyo kwa niaba ya msikiti wa Bakwata Buseresere, Shekhe wa Kata hivyo Ibrahimu Mtambo, amempongeza Mbunge huyo kwa kitendo cha kutoa huduma hiyo katika mwezi mtukufu wa Ramadhan na kwamba wataendelea kumwombea kwa mwenyezi Mungu ili amuimalishe katika uongozi wake.

Amesema kitendo hicho cha kiungwana kimewatia moyo mkuu kwa kuwa tangu kuanzishwa kwa msikiti huo hakuwahi kutokea Mbunge mwingine yoyote kutoa sadaka kama hiyo.

Kwa upande wake, Shekhe wa msikiti wa Nyakayondwa, Majaliwa Said, mbali na kumshukuru Mbunge kwa huduma hiyo, ameongoza dua maalumu ya kumwombea Lutandula ili asipatwe na mambo mabaya na husda za wanadamu.

Hata hivyo baadhi ya waumini wa dini hiyo kata ya Bwanga, wamemuomba Mbunge huyo kuendelea kusaidia makundi yote hasa ya kidini na kwamba wanaridhishwa na upendo anaoendelea kuuonyesha katika jamii hasa katika Jimbo hilo.