Miili watumishi wa afya waliofariki kwa ajali ya boti Kigoma, yaagwa

Kigoma. Wananchi, watumishi na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Kigoma wameaga miili ya watu saba waliokufa kwenye ajali ya boti. Huku wananchi wakisisitizwa kufuatilia taarifa ya hali ya hewa.

Miili iliyoagwa ni ya watumishi wanne wakiwamo muuguzi msaidizi, Paul Luvanda (29), tabibu wa afya, Rachel Msalila (28), tabibu wa kinywa na meno, Joyce Kandole (29) na mfamasia, Winny Nyabusani (31). Wengine ni Amos Sika (33), ambaye ni tabibu na mwili wake haujapatikana hadi sasa, na juhudi za kuutafuta zinaendelea. Wasaidizi watatu wa shughuli ya uandikishaji Bima ya Afya kwa Wote waliotambulika kwa jina moja moja ni Erick, Omary na Geofrey, ambaye alikuwa dereva bodaboda.

Watumishi hao walikuwa wakienda kwenye majukumu yao ya kazi kwa usafiri wa majini.

Baadhi ya wananchi wa mkoa wa Kigoma waliojitokeza kuaga miili ya wapendwa wao, katika kiwanja cha mpira cha Kazegunga leo Jumamosi, Machi 14, 2026.

 Ndugu wa marehemu, Magreth Aloyce, alisema binamu yake Erick alikuwa mtu mwenye upendo kwa watu na atamkumbuka kwa wema wake, kwani kila alipomaliza shughuli zake za kila siku alikuwa akipitia nyumbani kwao kuwajulia hali kabla ya kwenda kwake.

Akizungumza kwenye hafla ya kuaga miili hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro, aliwatahadharisha wananchi, hasa wale wenye shughuli zinazotegemea Ziwa Tanganyika, kufuatilia kila siku utabiri wa hali ya hewa kupitia vyombo vya habari ili kuchukua tahadhari stahiki.

Majeneza yenye miili ya watu saba waliokufa kwenye ajali ya boti Ziwa Tanganyika.

 “Mkoa umepoteza watu muhimu ambao walikuwa wakienda kuwatumikia wananchi. Ndugu zangu wafiwa, huu msiba sio wenu peke yenu, ni wa watu wote na wamekufa wakitetea maisha ya Watanzania, hivyo hii ni sababu tosha ya kujifariji nayo kama wafiwa,” alisema Sirro.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kila siku inatoa taarifa ya hali ya hewa kwenye vyombo vya habari ikieleza kuhusu hali ya mvua, upepo mkali, mawimbi makali, ngurumo na radi.

Sirro aliwataka wananchi kuchukua tahadhari hizo, kwani zinaweza kuokoa maisha na kuzuia ajali zinazoweza kutokea Ziwa Tanganyika, ambalo ndilo lenye kina kirefu zaidi barani Afrika, likifikia mita 1,470.

Kwa upande wake, mwakilishi kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Paul Chaote, alisema haiwezi kupingika kuwa ni msiba mzito, lakini amewataka watumishi waliobaki wajipe moyo na kuendelea kuchapa kazi kwa kulitumikia Taifa lao.

Mtumishi wa Halmashauri, Anita Katema, alisema alikuwa karibu na Rachel ambaye walikuwa na utaratibu wa kumpitia kila mara wanapokuwa wanaenda kutoa huduma kwa wananchi, hivyo msiba huo umemuumiza na hawezi kusahau kwa haraka.

Mkazi wa Kigoma, Shamimu Rajab, alisema watumishi hao walifika kwa lengo la kuwatumikia wananchi wa mkoa huo, lakini leo wanarejeshwa wakiwa wamefariki dunia.