Mwezi mmoja freshi kwa Kocha JKT Tanzania

KOCHA wa maafande wa JKT Tanzania, Ahmad Ally, amesema licha ya timu hiyo kukaa kwa zaidi ya mwezi mmoja bila ya kucheza mechi za kiushindani, ila haitaathiri programu mbalimbali za kikosi hicho, kutokana na mipango mikakati waliyoiweka.

Timu hiyo tangu mara ya mwisho ilipocheza na Yanga na kuchapwa mabao 5-0, Februari 25, 2026, haina mechi yoyote ya Ligi Kuu hadi Aprili 4, 2026, itakapokuwa kwenye Uwanja wa Majaliwa, Lindi, kucheza dhidi ya Namungo FC.

Akizungumzia mapumziko hayo, Ally amesema sababu kubwa ni kutokana na timu hiyo kucheza mechi nyingi haraka tofauti na ilivyokuwa kwa wapinzani wao, hivyo ni muda mzuri kwao wa kuendelea na programu mbalimbali hasa za utimamu wa kimwili.

“Tulicheza mechi nyingi mfululizo bila ya kupata muda mzuri pia wa kupumzika, kwa sasa ni zamu yetu kuendelea kufanyia kazi dosari zilizojitokeza hapo mwanzoni, ili tutakaporudi tuwe na nguvu mpya ya kushindana na wenzetu,” amesema Ally.

Kocha huyo amesema kwa kipindi cha mwezi mmoja na takribani wiki moja ambacho hawana mechi, wanakitumia kwa ajili ya kutengeneza muunganiko mzuri hasa eneo la ushambuliaji, ambalo kwa hivi karibuni limekuwa na changamoto kubwa.

“Ni kweli washambuliaji wengi wanapitia kipindi kigumu cha kutokufunga, lakini siwezi kusema ni wao peke yao kwa sababu kama hawafungi ni lazima eneo la kujilinda pia liwe bora, japo ukiangalia maeneo yote yanakosa hiyo balansi tunayotaka,” amesema.

Msimu huu timu hiyo imecheza mechi 17 za Ligi Kuu, ambapo kati ya hizo imeshinda saba, ikitoka pia sare saba na kupoteza tatu, ikishika nafasi ya pili na pointi 28, ikiwa nyuma ya mabingwa watetezi, Yanga iliyo kileleni na pointi 35.