Pedro Goncalves afichua hesabu mpya za Yanga

YANGA imerudi nyumbani ikijiandaa kucheza tena ugenini dhidi ya Azam FC, lakini ule mchezo dhidi ya Prisons ukampa akili mpya kocha wao, Pedro Goncalves na sasa amewatenganisha f’lani kimehesabu mastaa wake.

Iko hivi: Yanga ilipocheza juzi dhidi ya Prisons na kushinda kwa bao 1-0, goli lao lilitokea benchi dakika ya 61, alipoingia mshambuliaji Laurindo Aurelio ‘Depu’ akifunga dakika ya 78 kwa kumalizia mpira uliotemwa na kipa Mussa Mbissa kufuatia shuti la adhabu ndigo lililopigwa na Allan Okello.

Akizungumza na Mwanaspoti, Pedro alisema kwenye kila wachezaji wanaoanza na wale wanaokaa benchi huwa ni hesabu zao za kuwa na akili ya kukabiliana na mpinzani kwenye mechi zao, ambapo imekuwa inawasaidia.

Pedro alisema kwenye mchezo dhidi ya Prisons waliona kwamba wenyeji wao wameamua kuitafuta pointi moja, maamuzi ambayo kwao hawakutaka kukubaliana nayo na kubadilisha hesabu zao kwenye mpango wa uchezaji.

Pedro alisema hawakuwa na sababu tena ya kuendelea kujiimarisha kiulinzi na kumtoa kiungo mkabaji Mohammed Domaro na kumuingiza Depu, hatua ambayo iliwaweka kwenye wakati mgumu Prisons kuweza kuhimili presha yao.

“Kuna wakati ulikuwa unaona timu yao nzima ipo kwenye nusu yao, haikuwa rahisi sana kutengeneza nafasi nyingi tena, lakini tulikuwa tumemweka Depu nje na wengine kwa hesabu, na baadaye zikatusaidia,” alisema Pedro.

“Tulihitaji ushindi, na kama tukikutana na timu inayokaa nyuma kama hivi, tuna timu nzuri ambayo bado inaweza kufanya kitu tofauti kutengeneza nafasi.”

Akizungumzia hatma ya Pacome Zouzoua, Pedro alisema bado kiungo huyo anaendelea kuimarishwa sawasawa na timu ya utimamu wa mwili kabla ya kurudishwa kuanza kucheza mechi zinazoendelea.

“Pacome bado kidogo, kama ambavyo nilisema kabla, hatutaki kuharakisha kurudi kwake. Anaendelea kuimarishwa juu ya utimamu wake wa mwili. Nikiambiwa yuko sawa, atarudi kazini. Ni mchezaji muhimu mwingine kwetu ambaye kwenye mechi zilizopita tumemkosa.”

Pedro amelizwa na ratiba ngumu ya ligi, akisema kwa maoni yake ratiba ya ligi kwenye mechi zao ni ngumu, ambapo wanalazimika kucheza mechi kila baada ya siku mbili kutoka kwenye mchezo uliopita, ikiwanyima muda mzuri wa kupumzika na kujipanga.

Pedro alisema ratiba hiyo inawapa presha kubwa wao makocha, ambapo ikitokea wachezaji wakapata maumivu au kukumbana na mchoko, inaharibu kiwango cha timu kwa kukosa nafasi ya kurudisha miili yao kwenye utulivu.

“Kwa maoni yangu, kiukweli ratiba hii ni ngumu sana. Kucheza mechi kila baada ya siku mbili sio kitu rahisi. Unahitaji wachezaji wenye miili bora sana na akili ya kujua kuwarudisha kwenye hali ya utimamu wa mwili.

“Angalia tulicheza dhidi ya Simba, tukatakiwa baada ya siku mbili tuwe Singida. Hizo ni mechi zote ngumu. Tunarudi nyumbani, tunatakiwa kusafiri tena kuja Dodoma, tunacheza kwenye uwanja mgumu kidogo, tunarudi nyumbani, tuna siku mbili tu hapa za kuwapumzisha wachezaji na kujiandaa na mchezo mwingine mgumu dhidi ya Azam. Sisi Yanga tu tunakabiliana na hili.”