‘Piga nikupige’ yashika kasi Mashariki ya Kati

Dar es Salaam. Mashambulizi makali yameendelea kufanyika Mashariki ya Kati ambapo nchi zinazohusika moja kwa moja katika mapigano hayo zikishambuliana kwa majibizano.

Nchi za Marekani na Israel zilianzisha mashambulizi hayo dhidi ya Iran, nchi ambayo nayo haikusita kulipiza kisasi kwa kuishambulia Israel moja kwa moja na kuzilenga mali za Marekani zilizopo katika ukanda huo.

Hadi sasa, ikiwa ni siku ya 15 tangu mapigano yalipoanza Februari 28, 2026, takribani watu 1,300 wamepoteza maisha, maelfu wamejeruhiwa na wengine wakilazimika kuyahama makazi yao.

Miundombinu pamoja na makazi vimeharibiwa katika miji tofauti nchini Iran, Israel na Lebanon ambako Israel inawalenga wapiganaji wa Hezbollah.

Matumaini ya kumalizika haraka kwa vita hivyo yanazidi kufifia kutokana na kila upande kuzidi kujiimarisha kwa ajili ya mashambulizi zaidi, jambo ambalo linaloashiria kwamba mapigano hayo yataendelea kwa muda mrefu.

Leo, duru za kimataifa zinaonyesha kwamba mapigano yamekuwa ni kwa pande zote zinazohusika huku kila mmoja ukijibu mashambulizi na kusababisha madhara zaidi katika maeneo yaliyoshambuliwa.

Kundi la wanamgambo wa Lebanon, Hezbollah, limedai kutekeleza mashambulizi kadhaa usiku kucha kuamkia Jumamosi, dhidi ya Israel katika maeneo waliyoyalenga.

Katika mfululizo wa taarifa zake, kundi hilo limesema limerusha makombora mengi kuelekea Kiryat Shmona, mji wa Israel ulioko karibu na mpaka wa Lebanon, na pia kufanya mawimbi mawili ya mashambulizi dhidi ya mji wa Metula, kaskazini mwa Israel.

Pia, limedai kurusha mashambulizi ya makombora katika kambi ya kijeshi ya Ein Zeitim, karibu na mji wa Safad. Limesema limewalenga wanajeshi wa Israel mara mbili katika kijiji cha mpakani cha Odaisseh nchini Lebanon.

Katika shambulizi tofauti, kundi hilo limesema limewalenga wanajeshi wa Israel katika mji wa mpakani wa Blida na wengine karibu na kituo cha kizuizini kilichoko mji wa Khiam.

Wakati huohuo, Jeshi la Israel limesema katika taarifa fupi iliyochapishwa kwenye mtandao wa Telegram kuwa wanajeshi wake waliwabaini wapiganaji wa Hezbollah wakibeba makombora na kuyaingiza katika ghala la kuhifadhia silaha katika eneo la Majdal, lililopo katika Wilaya ya Tyre, kusini mwa Lebanon, jana Ijumaa.

Taarifa hiyo, imesema dakika chache baadaye jeshi hilo lilishambulia ghala hilo kwa njia ya anga Jumamosi na kuwaua wapiganaji hao.

Hata hivyo, jeshi hilo halikutoa maelezo zaidi kuhusu idadi ya watu waliouawa au kujeruhiwa katika shambulizi hilo.

Kwa miezi kadhaa kabla ya kuongezeka kwa mvutano wa hivi karibuni, Israel imekuwa ikifanya mashambulizi katika jamii kadhaa za kusini mwa Lebanon.

Shirika la Habari la Fars, linalohusishwa na Serikali ya Iran, limethibitisha kufanyika kwa shambulizi katika Kisiwa cha Kharg nchini humo, likisema maeneo yaliyolengwa ni pamoja na kituo cha ulinzi cha Jeshi la Iran, ngome ya jeshi la wanamaji, mnara wa kudhibiti helikopta na meli inayobeba helikopta.

Rais wa Marekani, Donald Trump amesema majeshi ya Marekani “yameangamiza kabisa” maeneo ya kijeshi ya Iran katika kisiwa cha Kharg, kisiwa muhimu kilicho karibu na pwani ya kusini-magharibi mwa nchi hiyo. Ameonya kwamba miundombinu ya mafuta katika kisiwa hicho, pia, itashambuliwa.

Kuhusu hatua za kujibu, Makao Makuu ya Jeshi la Iran yamesema iwapo miundombinu ya mafuta katika kisiwa cha Kharg itashambuliwa, Iran itajibu kwa kulenga vituo vyote vya mafuta au miundombinu ya nishati katika eneo la Ghuba, ambavyo vinahusiana kwa namna yoyote na Marekani.

Katika siku chache zilizopita, tayari kumeshuhudiwa mashambulizi ya Iran dhidi ya baadhi ya miundombinu hiyo, lakini hayakuwa makubwa kiasi cha kuvuruga kabisa shughuli au kuathiri pakubwa sekta ya mafuta katika nchi hizo.

Baadhi ya mashambulizi madogo yameripotiwa katika nchi za Saudi Arabia na Qatar, miongoni mwa maeneo mengine.

Sasa Iran inaonya uwezekano wa kuanzisha mashambulizi makubwa zaidi dhidi ya miundombinu hiyo pamoja na vituo vingine vya mafuta katika mataifa ya Ghuba, jambo ambalo linaweza kuwa na athari kubwa kwa eneo hilo na pia kwa sekta ya mafuta na gesi duniani.

Iran inaweka hatua hiyo kama karata ya mwisho. Kwa sasa imekuwa ikizungumzia kujizuia, lakini imeonya hali hiyo inaweza kubadilika iwapo miundombinu yake ya mafuta itashambuliwa, kama ambavyo Marekani imekuwa ikidokeza na kutishia kufanya.

Katika hatua nyingine, wanajeshi wa Marekani wa kikosi cha 31st Marine Expeditionary Unit, wameanza kuelekea eneo la operesheni kutoka bandari yao ya Okinawa, wakiwa pamoja na meli ya kijeshi ya USS Tripoli.

Hii ni meli maalumu ya mashambulizi ya majini ambayo hutumika kama kituo cha kupeleka wanajeshi wa majini katika eneo la mapigano, iwe kwa ajili ya kukabiliana na mgogoro au hata kupeleka vikosi vitakavyoweza kudhibiti sehemu fulani ya ardhi ya Iran, endapo hali itahitaji.

Kimsingi, wanatajwa kuwa wanajeshi wa kwanza wa ardhini wa Marekani wanaoelekezwa katika vita vinavyohusisha Marekani na Israel dhidi ya Iran. Wanamaji hao hufanya operesheni zao baharini na pia ardhini.

Hatua hiyo inaonyesha kuwa Marekani inaongeza taratibu uwepo wake wa kijeshi katika mzozo huo, jambo linaloashiria kuwa huenda vita hivyo visiishe haraka kama baadhi ya watu walivyotarajia.

Iran yashambulia ubalozi wa Marekani

Katika hatua nyingine, Ubalozi wa Marekani uliopo katika mji mkuu wa Iraq, Baghdad, umeshambuliwa kwa kombora.

Kwa mujibu wa chanzo cha usalama cha Iraq kilichozungumza na Al Jazeera Machi 14, 2026, kimesema shambulizi hilo liliharibu sehemu ya mfumo wa ulinzi wa anga wa ubalozi huo na moshi ulionekana ukifuka kutoka ndani ya eneo hilo.

Maofisa wawili wa usalama, pia, waliiambia Associated Press kuwa kombora moja lilipiga eneo la kutua helikopta (helipad) ndani ya ubalozi huo.

Kwa mujibu wa maofisa hao, kombora hilo lilitua ndani ya mipaka ya ubalozi uliopo Green Zone, kitongoji chenye ulinzi mkali katikati ya mji wa Baghdad ambako kuna taasisi za Serikali ya Iraq pamoja na balozi mbalimbali za nchi za kigeni.

Maofisa hao walizungumza kwa sharti la kutotajwa majina kwa kuwa hawana mamlaka ya kuzungumza na vyombo vya habari. Hadi sasa, ubalozi wa Marekani mjini Baghdad haujatoa taarifa rasmi kuhusu tukio hilo.

Mapema Ijumaa, ubalozi wa Marekani nchini Iraq ulirudia onyo lake la usalama, ukisema Iran pamoja na makundi ya wanamgambo yanayoungwa mkono na Iran, yamewahi kufanya mashambulizi dhidi ya raia wa Marekani, masilahi yake na miundombinu mbalimbali.

Wakati hayo yakitokea, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limesema limeiarifu Falme za Kiarabu (UAE) kuwa maeneo ambayo ni maficho ya wanajeshi wa Marekani ni “maeneo halali” ya kushambuliwa, kufuatia shambulizi la Marekani katika kisiwa cha Kharg nchini Iran.

Katika taarifa iliyosambazwa na shirika la habari la Iran la Tasnim, IRGC imesema inaona ni haki yake ya kisheria kulinda mamlaka na ardhi ya taifa hilo kwa kulenga maeneo ambako makombora ya Marekani yanatoka.

Taarifa hiyo imesema mashambulizi yanaweza kulenga bandari, magati ya meli pamoja na maeneo yanayodaiwa kuwa maficho ya wanajeshi wa Marekani katika baadhi ya miji ya UAE.

IRGC, pia imewataka wakazi wa UAE pamoja na watu wanaoishi karibu na bandari, magati ya meli na maeneo ya kijeshi ya Marekani, kuondoka ili kuepuka madhara, iwapo mashambulizi yatatokea.