Dar es Salaam. Mwili wa mwanadiplomasia na mwanazuoni nguli, Profesa Costa Mahalu umeagwa jijini Dar es Salaam, huku wanazuoni na wanasiasa wakimtaja kuwa miongoni mwa viongozi waliopenda kuibua vipaji na kuendeleza vijana waliokuwa vyuoni.
Mbali na hilo, wamesema Profesa Mahalu ambaye alikuwa Makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Mt Augustine (Saut) alikuwa mhamasishaji mnyenyekevu, mpenda haki, mpole, mwenye utu aliyeishi katika misingi ya taaluma yake ya sheria aliyoibobea.
Hayo yameelezwa leo Jumamosi Machi 13, 2026 baada ya misa ya kumuaga katika Kanisa la Mtakatifu Petro, Oysterbay jijini Dar es Salaam. Misa hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Elimu, Profesa Adolf Mkenda.
Wengine waliohudhuria ni Jaji Joseph Warioba, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, mabalozi wastaafu, John Cheyo (Mwenyekiti wa UDP), Spika wa zamani, Anne Makinda, Mama Anna Mkapa na Andrew Chenge.
Akitoa salamu kwa niaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Lauren Mussa amesema taasisi hiyo, itamkumbuka Profesa Mahalu kama mwanafunzi na mhitimu wa shahada ya awali ya sheria mwaka 1974.
“Chuo kitakumbuka Balozi Mahalu kama msomi aliyebobea katika sheria za kimataifa, hasa hasa sheria za masuala ya bahari, pia kama Amidi wa kitivo cha sheria kuanzia mwaka 1985/1986 – 1990/1991.
“Balozi Mahalu alifanikisha mengi ikiwemo kuwawezesha wafanyakazi wanataaluma waliokuwa chini yake kwenda masomo ya uzamivu ughaibuni,” amesema Dk Mussa.
Kwa mujibu wa Dk Mussa, walionufaika na uwezeshaji wa Profesa Mahalu ni pamoja na Profesa Palamagamba Kabudi (Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Kazi Maalumu), Dk Aggrey Mlimuka na Dk Harrison Mwakyembe.
Mbali na hilo, Dk Mussa amesema akiwa chuoni hapo, Profesa Mahalu alipendekeza kuajiriwa kwa wanataaluma wapya Profesa Bonaventure Rutinwa, Profesa lbrahim Juma, Jaji Robert Makaramba, Jaji Fauz Twaib, Profesa Sifuni Mchome na Profesa Hamudi Majamba
Kwa upande wake Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Herny Mchamungu amesema Profesa Mahalu aliishi maisha ya kugusa familia, jumuiya na umma, akihudumu kama mwanasheria, mwanadiplomasia na mkufunzi wa vyuo.
“Amehudumu si kama kazi bali kwa manufaa ya wote, kifo sio mwisho bali ni lango la kuingia maisha mapya. Balozi Mahalu alijaribu kutembea katika njia ya Kristo katika maisha yake,” amesema Askofu Mchamungu.
Amesema Profesa Mahalu alikuwa mtu mwema mwadilifu, msikivu na mkarimu kwa wote na imani inaeleza kuwa fanya kazi kwa masilahi ya wote, ndio wito ulitukuka.
Kwa upande wake, Jaji Warioba amesema anakumbuka Profesa Mahalu kwa namna alivyomshawishi kuendelea na kazi, licha ya kustaafu serikalini.
“Costa na mimi tulikuwa mtu na kaka yake au mtu na mdogo wake. Nilimsimamia Costa kwenye masomo yake, na mimi nilivyostaafu Serikali aliniomba niendelea kufanya naye kazi kwenye kampuni ya sheria.
“Aliniambia nikikaa bila kufanya kazi ubongo utakaganda, lazima niendelee kufanya kazi. Bila Costa ubongo wangu ungekuwa umeshaganda sasa, ingawa sasa hivi una butu, lakini yeye ndiye aliyesimamia akili yangu iendelee,” amesema Jaji Warioba.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (Mwauwasa), Neli Msuya amesema watamkumbuka Profesa Mahalu alikuwa mstari wa mbele kutoa ushauri wa kuongoza mamlaka hiyo.
Amesema Profesa Mahalu alikuwa mjumbe wa bodi wa mamlaka hiyo na alikuwa pia mstari wa mbele kuhakikisha haki inatendeke kwa kila mtumishi.
Naye, Profesa Mkenda amesema yeye na Profesa Mahalu walikuwa marafiki wa muda mrefu na walifahamiana Chuo Kikuu cha Dar es salaam na wamekuwa wakiwasiliana mara kwa mara.
“Tumekuwa tukitaniana na Balozi Mahalu, nakumbuka mwaka 2018 nikiwa katibu mkuu wa wizara ya mambo ya nje, nilipewa maelekezo na mamlaka nitangaze kuwa Mahalu anarudishiwa hadhi ya ubalozi.
“Kwa hiyo kila tukikutana alikuwa akinitania kuwa mimi ndiye nimemrudishia hadhi ile, lakini kiukweli mamlaka ndio iliyomrudishia, mimi nilitangaza tu,” amesema Mkenda.
Profesa Mahalu hadi umauti unamkuta alikuwa Makamu Mkuu wa Chuo cha Mtakatifu Augustine Mwanza, alifariki dunia Machi 9, 2026 katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) alikokuwa akipatiwa matibabu, amezikwa leo katika makaburi ya Kinondoni.
