“””””””
****
Serikali imeanzisha mpango maalumu wa kuwaandaa vijana kuwa wawekezaji wakubwa kwa kuwapa mafunzo ya uzalishaji wa kisasa na kuwaunganisha moja kwa moja na masoko ya kimataifa, hatua inayolenga kuimarisha biashara ya nje na kukuza uchumi wa viwanda nchini.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo.
Amesema mpango huo unaendana na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kujenga rasilimali watu yenye ujuzi mkubwa na kuifanya Tanzania kuwa mshindani katika soko la kimataifa.
Uzinduzi wa programu hiyo umefanyika katika Benjamin William Mkapa Special Economic Zone eneo la Mabibo, chini ya uratibu wa Tanzania Investment and Special Economic Zones Authority (TISEZA).
Kwa mujibu wa Profesa Mkumbo, awamu ya kwanza itahusisha vijana kati ya 30 na 50 watakaopatiwa mafunzo ya ujasiriamali, uendeshaji wa viwanda na mbinu za kisasa za uzalishaji na utafutaji wa masoko ya ndani na nje ya nchi.
Amesisitiza kuwa Tanzania ina nafasi ya kipekee ya kimaendeleo kwa kuwa zaidi ya asilimia 80 ya wananchi wake ni vijana wenye umri chini ya miaka 40, nguvu kazi ambayo ikitumika vizuri inaweza kuibadilisha nchi kiuchumi.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Fred Msemwa.
Naye Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Fred Msemwa amesema mpango huo ni sehemu ya mageuzi ya kiuchumi yanayolenga kuimarisha sekta ya uzalishaji na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara katika ukanda wa Afrika kupitia fursa za African Continental Free Trade Area (AfCFTA).












