Tacas yataka bandari iachane na ada mpya

Dar es Salaam. Chama cha Wakala wa Forodha Tanzania (Tacas), kimeiomba Serikali kuachana na mpango wa kutoza ada ya Uendelezaji wa Miundombinu ya Bandari (PID) na badala yake kutafuta vyanzo vingine mbadala vya mapato.

Chama hicho kimetoa ushauri huo ikiwa ni maazimio ya mkutano wa dharura wa kujadili ada hiyo, uliofanyika Machi 13 jijini Dar es Salaam, uliwakutanisha wajumbe kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Mwenyekiti wa Tacas, Efrahim  Mwankuse amesema wamelazimika kuitisha mkutano huo wa dharura ili kupata maoni ya wanachama kuhusu ada hiyo, kwa kuwa hakuna wanaloweza kulipeleka katika Serikali kama wanachama wao hawatalikubali.

Mwankuse amesema kupitia mkutanao huo, watafikisha hoja zilizoibuliwa na wanachama kwa Serikali na mwisho wa siku yenyewe itapima kama kuna haja ya kuendelea na maamuzi ya ada hiyo au la.

Mkutano huo wa dharura umeitishwa ikiwa imepita siku chache tangu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari  Tanzania(TPA),  Plasduce Mbossa atangaze kusitisha hadi Juni 30  utozaji wa ada hiyo iliyoanza Machi 8, 2026.

Mbossa alisema muda uliotolewa wa hadi Juni 30, 2026 utawapa wadau nafasi ya kurekebisha masharti ya mikataba yao ya kibiashara na wateja wa ndani na nje ya nchi, ili kuendana na matakwa ya ada hiyo.

Akichangia hoja kwenye mkutano huo wa dharura, Asmalita Mkufya, amesema suala hilo la ada limekuja ghafla na kuchangia kuharibu mahusiano na wateja wao.

Asmalita amesema, baada ya ada hiyo kutumika, mteja wake aliyepaswa kulipa ada ya Sh334,000, kutoa gari yake alijikuta akitakiwa kulipa zaidi ya Sh2 milioni, fedha ambazo haikuwa rahisi kuzipata kwa muda huo, wakati alikuwa tayari amemaliza kila kitu anasubiri kupokea mzigo wake.

“Jambo hili limepoteza uaminifu na wateja wetu, tunaonekana mawakala kama hela hiyo ni sisi tumeitengeneza, hivyo kuharibu uhusiano kati yetu na wao,” amesema Asmalita.

Naye Douglas Shayo, aliyeanza kazi hiyo ya uwakala  miaka ya 1986, amesema tozo hizo hazifai tu kwao mawakala bali kwa Watanzania wote, kwa kuwa zinakuja kupandisha gharama za utoaji mizigo na muumiaji wa mwisho ni mwananchi wa kawaida, ambaye atapandishiwa bei katika bidhaa atakayoinunua.

“Hili suala Serikali inatakiwa iwe nalo makini kwani naona wafanyabiashara wanaotumia bandari yetu watakavyotukimbia na kwenda bandari zingine nchi jirani, hivyo ni vema vikatafutwa vyanzo vingine vya mapato,” amesema Shayo.

Selina Kipangula, amesema kuna haja ya kuangaliwa upya kwa jambo hilo, na kuwa gari la mteja wake aliyekuwa amelinunua kwa Sh70 milioni, lilipofika nchini ametakiwa kulilipia tena Sh19 milioni kutokana na  ongezeko la ada na tayari amemwambia nia yake ya kutaka kuihama bandari ya Tanzania.

Moris Kabega amesema wazo hilo halitekelezeki na amemtaka aliyelipendekeza kuachana nalo, akieleza kuwa kwa hali lilivyo ni sawa na ushuru.

Pia, amekumbusha miaka ya nyuma namna wafanyabiashara walivyokimbia bandari ya Dar es Salaam kutokana na tozo kwenye vitenge, wateja ambao hadi leo wameshindwa kuwarudisha.

Deogratius Kanimba, amesema ni mara ya pili  kuahirishwa maamuzi ya utozaji ada hiyo na hawajawahi kupewa taarifa kuhusu sababu, hivyo ni vyema elimu zaidi ikatolewa kabla ya kufika hiyo Julai.