TMA yatoa tahadhari ya mvua kubwa, mafuriko

Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeonya kuwa mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika baadhi ya maeneo ya nchi zinaweza kusababisha mafuriko, kuharibu miundombinu na kuathiri shughuli za uvuvi katika maeneo ya pwani.

Taarifa iliyotolewa na TMA imetaja maeneo yanayotarajiwa kuathirika ni pamoja na mikoa ya Lindi, Mtwara, Pwani pamoja na visiwa vya Mafia, kulingana na taarifa ya mamlaka hiyo.

Katika utabiri wa siku tano wa athari za hali mbaya ya hewa uliotolewa na TMA kuanzia Machi 13 hadi 15, 2026, mamlaka hiyo imesema mvua za wastani hadi kubwa zinatarajiwa kunyesha katika maeneo kadhaa, hali inayoongeza hatari ya kutokea kwa mafuriko.

TMA imeeleza kuwa mvua hizo zinaweza kusababisha usumbufu katika shughuli za kijamii na kiuchumi pamoja na kuharibu miundombinu endapo wananchi hawatachukua tahadhari mapema.

“Jamii katika maeneo yanayotarajiwa kuathirika zinashauriwa kuwa makini na kuchukua tahadhari zinazostahili, kwani mvua hizi zinaweza kuathiri shughuli za kila siku pamoja na miundombinu,” imeeleza sehemu ya taarifa ya mamlaka hiyo.

Aidha, TMA imewataka wananchi, hususan wanaojishughulisha na shughuli za baharini kama uvuvi na usafiri wa majini, kufuatilia kwa karibu taarifa rasmi za hali ya hewa ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.

“Wananchi wanapaswa kuwa tayari na kuendelea kufuatilia taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na mamlaka ili kuepuka madhara makubwa,” imeongeza taarifa hiyo.