Wafanyabiashara Watakiwa Kulipa Kodi kwa Hiari Kuchochea Maendeleo

Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando, ametoa wito kwa wafanyabiashara kuendelea kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi kwa hiari ili kuchangia maendeleo ya nchi kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Akizungumza wakati wa futari iliyoandaliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Machi 13, 2026 jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, Msando amesema ni wajibu wa kila mwananchi kushiriki katika kulipa kodi ili kuiwezesha serikali kutekeleza majukumu yake ya maendeleo.

Aidha, amewahimiza wananchi kudai risiti wanapofanya manunuzi na wafanyabiashara kutoa risiti wanapouza bidhaa au huduma, akisisitiza kuwa hatua hiyo inasaidia kuongeza uwajibikaji katika ukusanyaji wa mapato ya serikali.

Msando pia ameipongeza TRA kwa kazi nzuri ya kutoa elimu ya kodi kwa wananchi katika ngazi mbalimbali, akieleza kuwa juhudi hizo zimechangia kuongeza uelewa kwa walipakodi na kupunguza malalamiko kutoka kwa wananchi.

Kwa upande wake, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Juma Mwenda, amesema taasisi hiyo ina matarajio kuona wananchi wanaendelea kuwa waadilifu na kuwajibika kwa hiari katika kulipa kodi, akisisitiza kuwa ulipaji kodi unapaswa kuwa sehemu ya ibada.

Mwenda amesema kupitia juhudi za TRA za kuhamasisha wananchi kufuata sheria za kodi, anaamini kuwa watu wengi wataendelea kuonesha uadilifu na uwajibikaji katika kulipa kodi kwa hiari.

“Ni matarajio yetu kuwa kadiri tunavyoendelea kuhamasisha watu kufuata sheria, wananchi wataendelea kuwa waadilifu na kuwajibika kwa hiari katika kulipa kodi kama sehemu ya ibada,” amesema Mwenda.

Naye Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zuberi, amewapongeza watumishi wa TRA kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kukusanya kodi kwa uadilifu na mafanikio, huku akiwashauri kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa haki na uadilifu kwa walipakodi.

Akizungumza katika futari hiyo iliyofanyika Dar es Salaam, Sheikh Zuberi amesema maadili ni nguzo muhimu katika mchakato wa ukusanyaji wa kodi na maendeleo ya taifa kwa ujumla.

Aidha, amewataka Watanzania kuendelea kuliombea taifa ili liendelee kuwa na amani na utulivu, huku akisisitiza umuhimu wa kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ili Mwenyezi Mungu aendelee kumpa hekima na nguvu katika kuliongoza taifa.

Sheikh Zuberi amesema kipindi cha mwisho cha mwezi mtukufu wa Ramadhani ni muhimu kwa waumini kuongeza ibada, kufanya dua na kujinyenyekeza kwa Mwenyezi Mungu ili awajaalie maisha mema na riziki zilizo halali na zenye baraka.

Pia amewahimiza wananchi kuendelea kuwa waaminifu katika kazi zao, akisisitiza kuwa uaminifu na uadilifu ni miongoni mwa ibada kubwa zinazomfanya mtu apendwe na Mwenyezi Mungu.