Wajane Rukia na Habiba, wanaopambana na mawimbi kutafuta riziki 

Dar es Salaam. Jua la asubuhi linaanza kuchomoza juu ya ufukwe wa Kawe Beach, mawimbi yakigonga kwa utulivu mchanga wa bahari. Ni katika eneo hilo ninaposubiri kwa zaidi ya saa tatu, nikitazama kwa makini kina cha maji ambako wavuvi wamezagaa wakitafuta riziki.

Lakini kati ya wote waliopo baharini, macho yangu yanavutiwa zaidi na wanawake wawili walioko ndani ya maji wakivua samaki.

Hao ni Rukia Abdallah na Habiba Rashid. Tofauti na wavuvi wengine wengi ambao ni wanaume, wao wapo peke yao kama wanawake, wakipambana na mawimbi kwa nyavu mikononi. Wakiwa wamejikita katika kazi yao, hawaonyeshi dalili ya uchovu wala woga, kana kwamba bahari imekuwa sehemu ya maisha yao ya kila siku.

Nikiwa pembezoni mwa ufukwe huo nikisubiri watoke majini ili nifanye nao mahojiano, ninashuhudia pia wachuuzi kadhaa wakisubiri wavuvi warejee ili wanunue samaki kwa ajili ya kuuza. Wengi wao ni wanawake.

Katika mazungumzo ya hapa na pale, wachuuzi hao wananieleza kuwa wanawake hao si wageni katika ufukwe huo. Wamekuwa wakifanya kazi ya uvuvi kwa miaka mingi kiasi kwamba wamezoeleka na kila mtu.

“Hawa kinamama tumekuwa nao hapa kwa muda mrefu sana. Hii ndiyo kazi yao miaka nenda rudi. Tumeshawazoea kabisa na kokote ukiwaona lazima wawe wawili kama unavyowaona kule ndani ya maji,” anasema mchuuzi mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Hadija.

Mchuuzi mwingine, Zainabu Hassan anasema kila anapofika ufukweni hapo, hupenda kununua samaki kutoka kwa wanawake hao.

Anasema anawathamini kwa sababu wamechagua njia tofauti ya kujitafutia kipato katika mazingira ambayo mara nyingi huchukuliwa kuwa ya wanaume.

“Unajua sisi wanawake tuna majukumu mengi. Mwanaume akirudi nyumbani kutoka kazini anaweza kupumzika, lakini mwanamke bado anakutana na kazi nyingine za nyumbani kama kupika, kusafisha na kulea familia. Nikiwa nawaunga mkono wenzangu hawa, nafanya hivyo pia kuwasaidia wapate kipato mapema ili warudi nyumbani kufanya majukumu yao mengine,” anasema.

Baada ya muda mrefu wa kusubiri, hatimaye saa 5:15 asubuhi inawadia. Ni muda wa wavuvi wengi kutoka baharini, wanawake hao wawili nao wanarejea ufukweni wakiwa wamebeba nyavu na samaki wachache waliowapata.

Wanapofika nchi kavu wanaketi chini na kuanza kuwachambua samaki, wakitoa uchafu uliokwama kwenye nyavu.

Ninajisogeza karibu na kujitambulisha. Hata hivyo, kwa mwonekano wa awali wanaonekana kuwa na hofu kidogo. Wananiuliza kwa nini nimewafuata, nataka nini kwao na kama kuna mtu amenituma.

Natumia muda kuwaeleza sababu ya kuzungumza nao. Ninawaambia kuwa dunia inaadhimisha Siku ya Wanawake Duniani na kazi wanayoifanya wao ni ya kipekee kiasi kwamba natamani kusikia hadithi yao, walivyoanza, changamoto wanazokutana nazo na ndoto zao za baadaye.

Baada ya maelezo hayo, Rukia Abdallah, mwenye umri wa miaka 60, anaanza kueleza safari yake ya maisha.

Anasema alianza kufanya kazi ya uvuvi takribani miaka 20 iliyopita baada ya kufiwa na mume wake.

Anasema kifo cha mume kilimuacha na mzigo mkubwa wa familia. Alibaki na watoto watano waliokuwa bado wanahitaji malezi, chakula na elimu.

“Nilipofiwa na mume wangu aliniacha na watoto watano. Nilikaa nikajiuliza nitawaleaje hawa. Mwanzoni nilikuwa nakuja hapa baharini kununua samaki na kwenda kuuza, lakini baadaye nikaona faida yake ni ndogo. Ndipo nikachukua uamuzi wa kuingia mwenyewe ndani ya maji kuvua,” anasema Rukia.

Anasema tangu wakati huo, kazi hiyo imekuwa tegemeo lake kuu la maisha.

“Kupitia uvuvi nimepeleka watoto shule na kuwapatia mahitaji muhimu ikiwamo chakula, na mpaka sasa licha ya umri wangu mkubwa bado ninavua samaki kwa sababu ndiyo kazi niipendayo,”anasema Rukia.

 Kuhusu kufanya kazi hiyo hata baada ya watoto wake kuwa wakubwa anasema, “maisha ni magumu. Huwezi kukaa ukasubiri mtoto akupe pesa wakati yeye pia ana majukumu yake. Akitoa sawa, asipotoa pia sawa. Ilimradi bado nina nguvu na mikono yangu miwili, nitaendelea kufanya kazi mpaka Mungu atakaposema basi kwani kutafuta hela kwa jasho lako kunaleta faraja na heshima.”

Kwa upande wake, Habiba Rashid anasema alianza kazi hiyo takribani miaka 10 iliyopita, akishawishiwa na rafiki yake Rukia.

Anasema na yeye baada ya kufiwa na mume wake, alijaribu kujitafutia kipato kwa kuuza mahindi ya kuchoma. “Nilikuwa nauza mahindi ya kuchoma, lakini kupata Sh10,000 ilikuwa kazi kubwa. Wakati mwingine ilichukua hata wiki nzima na bado mahindi yalikuwa hayaishi,” anasema Habiba.

Anasema siku moja Rukia alipomuona akihangaika, alimshauri ajiunge naye katika kazi ya uvuvi.

“Huyu rafiki yangu aliniambia Sh10,000 ambayo nilikuwa nikipata kwa wiki, naweza kuipata kwa siku moja nikivua samaki kwa sababu kitoweo hicho kinahitajika sana,” anasema.

Anasema ushauri huo ulimshawishi na tangu wakati huo, akaanza kufanya kazi ya uvuvi.

Leo hii, anasema kazi hiyo ndiyo inayomuwezesha kuendesha maisha yake, kuanzia wakati alipokuwa hana wajukuu mpaka sasa tayari ana wajukuu anaosaidia kuwalea.

Kama ilivyo kawaida kila kazi haikosi changamoto, kwa upande wao wanasema kubwa ni kutumia zana duni za uvuvi. Tofauti na wavuvi wengine wanaomiliki mitumbwi na nyavu za kisasa. Ambapo kuna wakati hutumia chandarua za kuzuia mbu kama nyavu za kuvulia samaki kwa sababu hawana uwezo wa kununua nyavu halisi.

Changamoto nyingine ni kushindwa kufika katika kina kirefu cha maji kutokana na kutokuwa na ujuzi wa kuogelea.

Habiba anasema maji yakifikia shingoni hulazimika kurudi nyuma, jambo linalowafanya kuvua samaki wachache waliopo karibu na ufukwe.

Aidha, anasema hawana mavazi maalumu ya kujikinga wanapokuwa majini. Kutokana na hali hiyo, wakati mwingine hukanyaga chupa zilizovunjika, miba au vitu vyenye ncha kali.

“Wakati mwingine tunajichoma sana, lakini kwa sababu ni katika utafutaji tunajitibu tu kienyeji na maisha yanaendelea,” anasema Habiba.

Pamoja na changamoto hizo, wanawake hao bado wana matumaini makubwa ya kubadilisha maisha yao. Ndoto yao kubwa ni siku moja kumiliki boti ya kuvulia samaki.

 “Kama unavyoona umri wetu umeenda. Kama tungewezeshwa kuwa na boti yetu ya kuvua, tunaweza kuajiri watu wakatuletea samaki kwa sababu tayari tunalijua soko vizuri. Hiyo ingekuwa nafuu kwetu,” anasema Habiba.

Anasema anatumaini pia ndoto hiyo inaweza kuwafikia viongozi, hasa Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye wanaamini anaelewa changamoto za wanawake wanaojitafutia kipato.

“Rais Samia ni mwanamke mwenzetu. Tunaamini anaelewa changamoto za wanawake na wajane kama sisi. Tungetamani kusaidiwa kupata boti ili tupumzike kidogo na kucheza sana na maji ya bahari,” anasema.

Kwa mujibu wa Augustino Richard, mmoja wa wavuvi katika eneo hilo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wavuvi wa Kawe Beach, wanawake hao wanastahili kupongezwa kwa juhudi zao.

Anasema licha ya ujasiri wao, mazingira wanayofanyia kazi ni magumu na yanahitaji msaada.

“Hawa wanawake wanafanya kazi hii kwa sababu ya shida, lakini ukweli ni kwamba mazingira ya baharini si rahisi. Kama kuna watu watasoma hadithi yao, ni vizuri wakasaidiwa mitaji au hata kununuliwa boti,” anasema.

Juma Kassim, naye ni mvuvi katika eneo hilo, anasema jamii inapaswa kuwapa msaada ili waweze kuboresha maisha yao.

Anasisitiza kuwa wanawake wanaweza kufanya kazi yoyote kama wanaume, lakini mazingira ya baharini yana changamoto nyingi.

“Hakuna sheria inayokataza wanawake kuvua. Tatizo si kwamba hawawezi, bali mazingira ya kazi yenyewe ni magumu,” anasema.