ALLIANCE Girls imeingia kambini rasmi Ijumaa kuanza maandalizi ya Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania inayotarajiwa kurejea April 03, huku uongozi wa timu hiyo ukianza mchakato wa kusaka kocha mkuu mpya atakayeiongoza kikosi hicho katika mzunguko wa pili.
Mabadiliko hayo yanafanyika katika benchi la ufundi kufuatia aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Sultan Juma kuondoka baada ya mkataba wake kutamatika katikati ya msimu.
Kiongozi mmoja kutoka klabuni hapo alisema kuingia kambini mapema ni sehemu ya kuimarisha maandalizi ya timu kabla ya kurejea kwa ligi.
“Wachezaji tayari wako kambini ili kuanza maandalizi mapema kwa ajili ya mechi zijazo. Tunajua ushindani wa ligi ni mkubwa hivyo tunahitaji kujiandaa vizuri,” alisema.
Alliance Girls itamaliza mechi ya kiporo cha mzunguko wa kwanza dhidi ya mabingwa watetezi JKT Queens Machi 27 kabla ya kukutana na Fountain Gate Princess Aprili 03.
“Tunajua tuna michezo miwili muhimu mbele yetu na hatuna kocha, hivyo tuko kwenye mchakato wa haraka wa kutafuta na maandalizi haya yatatusaidia kurejea kwenye ushindani na kupata matokeo mazuri,” alisema.
Hata hivyo, aliyekuwa kocha wa timu hiyo Sultan amekabidhi rasmi ripoti ya benchi la ufundi kwa uongozi wa klabu hiyo ikiwa ni sehemu ya kukamilisha mchakato wa mabadiliko ya benchi la ufundi.
“Tunafanya taratibu za kumpata kocha mpya. Tukikamilisha mchakato huo tutamtambulisha pamoja na benchi lake la ufundi.”