Askofu Massawe aonya upofu wa roho

Dar es Salaam. Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Arusha, Isaac Massawe amesema upofu wa roho umewafanya binadamu kujiona wapo juu ya Mungu hivyo kutojali haki za watu wengine.

Amesema mwanadamu hupofushwa na tamaa za mwili, mali na madaraka, hivyo kunahitajika mwanga wa kumsaidia kuona kwa usahihi na kutenda yaliyo sahihi.

Askofu huyo alitoa kauli hiyo leo Jumapili, Machi 15,2026 katika Misa Takatifu ya kumuaga Askofu Prosper Lyimo aliyekuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Arusha.

Kuagwa kwa kiongozi huyo kunakuja baada ya kuteuliwa kuwa askofu wa kwanza na mwanzilishi wa jimbo jipya la Bariadi baada ya uteuzi wake uliofanywa Januari mwaka huu na Kiongozi wa Kanisa Katoliki, Baba Mtakatifu Leo XIV.

Askofu Massawe amesema kipofu hutembea gizani usiku na mchana na katika hali hiyo anaweza kujiumiza kwa kukanyaga vitu vibaya.

“Kipofu anaweza kuumiza wengine na kukwaza. Upofu wa roho unamfanya binadamu kujiona yuko juu ya Mungu na kutojali haki za wengine.

“Kuharibu wengine na kuvuruga nafasi za huduma ni aina ya upofu, mwanadamu hupofushwa na tamaa za mwili, mali na madaraka, hivyo kunahitajika mwanga wa kuona sawa sawa na kutenda kwa usahihi,” amesema.

Askofu Massawe amesema Yesu alikuja duniani ili binadamu aishi katika ukweli na uhuru, akieleza kuwa Mungu hataki wanadamu wawe watumwa bali wawe watu wanaochagua njia sahihi na kuifuata kwa uaminifu.

Amesema upofu unaweza pia kusababishwa na ajali, kudhuriwa na watu wenye nia mbaya au kudanganywa kwa maneno ya uongo hadi kufikia hatua ya kuapa mahakamani bila kusema ukweli.

“Tunadanganyana katika nafasi mbalimbali, tunasema uongo na hata kuapa mahakamani kuwa tutasema ukweli na ukweli mtupu, lakini katika mioyo na akili zetu tunakuwa waongo wakubwa na kuwafanya wengine wapofushwe kwa taarifa za uongo,” amesema.

Amesema wapo watu wanaojigamba kuwa wakatoliki kwa muda mrefu na kudhani wanajua kila kitu, lakini inapofika wakati wa kushuhudia imani yao wanakuwa kama vipofu wasiojielewa.

Katika Injili, Askofu Massawe amesema waliotajwa kuwa vipofu si wale waliozaliwa na upofu, bali mafarisayo na waandishi waliodhani wanaona kumbe hawaoni.

Amesema mtu anayesema anaona ilhali yuko katika upofu basi ni kipofu kweli, kwa sababu matendo yake hudhihirisha hali aliyonayo.

Askofu huyo, amesema Mungu aliumba nuru kwa sababu bila nuru kungekuwa na fujo, kusingekuwa na maendeleo wala mpangilio, ndiyo maana kristo alifufuka ili binadamu asiishi katika uongo bali katika mwanga na kutenda yaliyo sahihi.

Amesema Yesu alidhihirisha kuwa yeye ni mwanga wa dunia alipomponya mtu aliyezaliwa na upofu, akifafanua kuwa asiyeona hubaki kusimuliwa yale asiyoyaona.

“Tamaa kubwa ya kipofu kuliko yote ni uwezo wa kuona, tusidhani uwezo wa kuona ni kitu cha kawaida, zawadi ya Mungu ni mwanga wa ndani na wa nje na tunapomuona mtu kipofu ni wajibu wetu kumsaidia.

“Inawezekana tunacheka vipofu, viwete na watu waliopata changamoto za maisha,tunamcheka huyu au yule, lakini mara nyingi hayo tunayafanya kwa upofu wetu,” amesema.

Akinukuu Zaburi ya 23, Askofu Massawe amewataka watumishi wa Mungu wanapoimba zaburi hiyo waelewe maana yake, akihoji kwa nini baadhi ya watu bado wanakwenda kwa waganga wa kienyeji, mizimu au kuruka ruka makanisa.

Amesema katika zaburi hiyo imeandikwa: “Bwana ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu,” akijiuliza kwa nini bado baadhi ya waumini wanaonesha kutokuwa na imani kamili kwa Mungu.

Akitoa salamu za pongezi kwa Askofu Mteule Lyimo, Makamu Askofu Katoliki Arusha, Saimon Tengesi amesema wananchi wa Bariadi wamepata kiongozi mwenye uwezo.

“Baada ya muda mtamshukuru Mungu kwa kweli kuwa mmepata jembe,” amesema.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Walei Jimbo la Arusha ambaye hakutaja jina lake  amempongeza askofu huyo kwa kuteuliwa katika nafasi hiyo.

 “Walei wote tunaahidi kukuombea ili uendelee kupata afya njema na kutekeleza majukumu yako kwa ufanisi,” amesema.

Katika pongezi hizo, alimkabidhi Askofu Lyimo zawadi kwa niaba ya walei wote akisema itamsaidia katika utekelezaji wa majukumu yake ya kichungaji.