KUNA mechi kubwa itapigwa Jumapili hii Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam ambapo wenyeji Azam FC watakapokutana na bingwa mtetezi wa Ligi Kuu Bara Yanga, nenda kaone ufundi mwingi kwenye dabi hiyo ya Dar es Salaam.
Mchezo huo utakuwa wa kwanza msimu huu kwa timu hizo kukutana kwenye ligi lakini kama unavyofahamu hakuna mchezo rahisi baina ya timu hizo kutokana na ushindani mkubwa zinapokutana.
Ndani ya mchezo huo, ngoja tukupe bato saba ambazo zitatokea ndani ya vikosi hivyo viwili, zipo zile za wachezaji uwanjani ambao kama wakipangwa hivyo kutakuwa na moto lakini hata mambo ya kiufundi.
Wenyeji wa mchezo huo Azam kinara wao wa mabao ni fundi Feisal Salum ‘Fei Toto’ akiwa na mabao sita mpaka anapoingia kwenye mechi ya leo, kiungo huyu atahitaji kuwakimbia wenzake kwa kufunga bao au mabao ili azidi kupaa kwa ufungaji.
Kule Yanga vinara wa mabao ni washambuliaji Prince Dube na Laurindo Aurelio ‘Depu’ wote wakifunga mabao sawa na yale ya Fei Toto ambapo mmoja au wote wakifunga kwenye mechi hii itakuwa ni kama wameongeza kasi ya kumfuata Fabrice Ngoy anayeongoza kwa ufungaji akiwa na mabao nane.
Azam chini ya kocha Florent Ibenge anakwenda kukutana na Yanga chini ya Pedro Goncalves kwa mara ya pili msimu huu baada ya awali kukutana kwenye fainali ya Kombe la Mapinduzi 2026 na Yanga kuchukua taji hilo kwa matuta ikishinda 5-4.
Haikuwa rahisi fainali hiyo ya Mapinduzi na sasa wawili hao wanakwenda kuonja joto la mchezo huo wakiziongoza timu zao kwenye ligi ambapo mbinu za kocha yeyote kati ya hao akipata ushindi zitakwenda kuiimarisha mbio za kusaka ubingwa msimu huu.
Ukiacha hilo Ibenge atataka kulipa kisasi cha kufungwa kwenye Kombe la Mapinduzi lakini pia Pedro atataka kuthibitisha kwamba hakubahatisha kuchukua kombe mbele ya Mkongomani huyo.
ZIDANE/KITAMBALA VS BACCA/MWAMNYETO
Safu ya ushambuliaji ya Azam inaweza kuongozwa na washambuliaji wawili, Zidane Sereri na Jephte Kitambala, mmoja kati ya hawa anaweza kuanza kwenye kikosi cha kwanza.
Kitambala amepoteza fomu yake kwa sasa akiwa na mabao mawili huku kocha wake akimuanzisha kutokea benchi kwe-nye mechi nyingi ingawa nguvu zake zinaweza kuwa mwiba mbaya kwa mabeki wa Yanga kama akianzishwa.
Zidane anapewa nafasi kubwa kutokana na morali yake akitoka kufanya vizuri kwenye mechi iliyopita dhidi ya Dodoma Jiji akifunga na kutoa asisti, kasi yake na ubora wa kufunga endapo akianzishwa atakuwa kwenye bato kubwa na mabeki wawili wa Yanga nahodha mkuu Bakari Mwamnyeto na Ibrahim Hamad ‘Bacca’ ambao sasa wanacheza pamoja tangu kuumia kwa Dickson Job.
Wakati kipa wa Yanga Djigui Diarra akichukua tuzo ya kwanza ya kipa bora wa msimu aliichukua kutoka kwa Aishi Manula wakati huo akiitumikia Simba, sasa wanakwenda kukutana tena wote wakiwa kwenye kiwango bora.
Diarra amecheza jumla ya mechi 10 za ligi msimu huu akikusanya jumla ya klinishiti nane kama sio shida ya kiafya ni wazi kwamba kipa huyo raia wa Mali atakuwa golini dhidi ya Azam akitafuta mchezo mwingine bila kuruhusu bao wakati Manula akicheza mechi tano tu kwenye ligi akiwa na klinishiti nne wakati kipa anayepokezana naye Zuber Foba akicheza naye mechi tano na zote akitoka na klinishiti.
FUENTES/YORO VS DUBE/DEPU
Safu ya ushambuliaji ya Yanga itaongozwa na mshambuliaji mmoja kati ya hawa, Prince Dube na Laurindo Depu kulingana na mfumo wanaoutumia ingawa yeyote atakayeanzia nje ana nafasi kubwa ya kuingia baadaye kuipigania timu hiyo.
Kumbuka washambuliaji hao wawili wote wana mabao sita kila mmoja ambapo watakuwa chini ya ulinzi wa mabeki wawili, Fuentes Mendoza na Yoro Diaby ambao watakuwa na jukumu kuhakikisha hawaendelezi rekodi , ya kufunga.
Yanga kama kuna mchezaji hawataki kusikia anawafunga leo ni Fei Toto ambaye alihamia Azam akitokea kwao tena kwa jeuri kubwa iliyozusha mivutano kwa klabu hizo mbili, hivi juzi wakati alipoonyeshwa kadi nyekundu kwenye mchezo dhidi ya Pamba Jiji, mashabiki wa Yanga kwa kiasi fulani waliumia kusikia jamaa atakuwa amemaliza adhabu yake na atakuwa uwanjani kwenye mechi hii.
Azam nao kama kuna mchezaji leo hawataki kumsikia akiwafunga basi ni Dube ambaye naye alihamia Yanga kama sehemu ya kulipa kisasi kufuatia Fei Toto kusajiliwa na matajiri wa Chamazi, habari ya kuvutia ni kwamba wawili hawa wote wana mabao sita na kila mmoja akiwa kwenye kiwango bora.
Fei Toto tangu ahamie Azam ameshawafunga Yanga na akifanya hivyo leo itakuwa ni muendelezo lakini Dube naye ameshawaliza mabosi wake wa zamani kama akifanya hivyo ni muendelezo tu sasa nani atakuwa na ubabe tutaona baada ya dakika 90.
Baada ya mchezo huo kumalizika itaanza mechi nyingine nje ya uwanja ikitua kwa wasemaji sasa kule Yanga kuna msemaji wao Ally Kamwe ambaye matokeo ya timu yake kushinda itakuwa ni kama nongwa kubwa kwa wapinzani wao.
Kule Azam nako kuna watu wawili ambao ni wasemaji, Thabit Zakaria ‘Zaka za kazi’ na Hashim Ibwe ambao kama timu yao itashinda huo utakuwa moto mbaya kwa mashabiki wa Yanga kwa kuandamwa na maneno ya kejeli.