KATIKA Ligi Kuu ya Zanzibar (ZPL), bado waamuzi wameendelea kuteseka kwa kuchezea vipigo kutoka kwa mashabiki, viongozi na hata wachezaji.
Hata hivyo, Bodi ya Ligi Zanzibar, imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuwafungia mashabiki na viongozi wa timu kushiriki katika mashindano yoyote yanayoandaliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu (ZFF).
Licha ya adhabu hizo, lakini sio suluhisho la moja kwa moja japo inaonesha njia na mwanga wa kuwathamini waamuzi wa ligi hiyo licha ya maslahi madogo wanayopata.
Hivi karibuni, Bodi hiyo iliitoza faini ya Sh5 milioni timu ya Zimamoto kwa kosa la baadhi ya wachezaji na viongozi kufanya vurugu na kupiga waamuzi wakati wa mchezo jambo lililosababisha kuvunjwa kwa mchezo huo dakika ya 75.
Hilo pekee halikutosha, Bodi hiyo iliitoza faini tena timu hiyo ya Sh250,000 za gharama ya matibabu kwa waamuzi waliothirika.
Viongozi watatu wa benchi la ufundi la timu hiyo akiwamo Kocha Msaidizi, Juma Abdulrahman, Kocha wa makipa, Hassan Ame na Meneja wa timu hiyo, Juma Othman walikutana na rungu la kufungiwa kufundisha na kuongoza mpira kwa misimu miwili. Pia wachezaji sita wa Zimamoto wamefungiwa kwa mwaka mmoja kucheza mechi zitakazoandaliwa na ZFF. “Wachezaji hao ni Abdullatif Shauri, Koffy Hamza, Nassor Mrisho, Omar Thani, Abdul-hamid Ramadhan na Suleiman Said,” ilisema taarifa hiyo ya Bodi.
Kiongozi Mwandamizi wa Zimamoto, Simai Tano, amefungiwa kujihusisha na mpira wa miguu ikiwemo kuhudhuria viwanjani kutazama michezo itakayoandaliwa na ZFF kwa kipindi cha miaka miwili.
Sura ya 20, (1), (2) na (3), sura ya 21 (6) na sura ya 28 (2), ya Kanunia ya mashindano toleo la 2025-2026 imeeleza kuwa ghasia, vurugu na kupigwa kwa waamuzi ni kosa kisheria.
Hata hivyo, Bodi hiyo inaendelea kuwasihi mashabiki, viongozi, wachezaji na makocha kuchunga nidhamu viwanjani ili kudumisha maslahi ya mpira wa miguu.