INAELEZWA Ceasiaa Queens imemwongeza aliyewahi kuwa kocha mkuu wa Alliance Girls, Sultan Juma kukiongoza kikosi hicho kuelekea mzunguko wa pili wa Ligi ya Wanawake.
Kabla ya kuifundisha Alliance Sultan alihudumu kwenye kikosi cha Geita Queens lakini timu haikufanya vizuri ikashuka daraja.
Chanzo kililiambia Mwanaspoti Sultan amesajiliwa kama kocha mkuu kuchukua nafasi ya Ezekiel Chobanka ambaye atakuwa msaidizi wake.
Ceasiaa imefanya hivyo kutokana na Chobanka ana leseni C ya ukocha hivyo atashindwa kusimamia mechi na imemwongeza Sultan ambaye ana leseni B.
“Sultan ni kocha mzuri hivyo tumaeamua kumwongeza kwenye timu kusaidiana na Chobanka ambaye ana leseni daraja C ya ukocha, ni uamuzi ambao utakuwa na manufaa kwetu,” kilisema chanzo hiko.
Ceasiaa iko kambini mkoani Iringa na inaelezwa kocha huyo ataanza majukumu yake leo Jumatatu.
Mwanaspoti ilipomtafuta Sultan kuzungumzia suala hilo hakupokea simu hata baadhi ya viongozi wa timu hiyo simu zao hazikupatikana.
Sultan alitimka Alliance hivi karibuni akiiacha timu ikiwa nafasi ya nne na pointi 19 tofauti ya pointi moja na bingwa mtetezi JKT Queens.
Mechi yake ya kwanza itakuwa Aprili 3, wakati Ceasiaa Queens watakapowakaribisha Geita Queens katika mchezo wa kwanza wa mzunguko wa pili utakaochezwa Uwanja wa Samora.