KOCHA Mkuu wa Simba, Steve Barker siku zinavyozidi kwenda, anapata jeuri kubwa ya kuendelea kufanya vizuri na kikosi hicho akiamini kina nafasi kubwa ya kufikia malengo msimu huu.
Jeuri ya Barker inakuja kwa kile alichoeleza kwamba, kikosi chake kinazidi kuimarika hali ambayo inampa wakati mzuri wa kuandaa timu ya kucheza na mpinzani yeyote huku akisema malengo ya kubeba ubingwa yapo palepale.
Akizungumza na Mwanaspoti, Barker amesema kwa sasa jambo zuri ni kwamba kikosi hicho kina sura mbili, kuna wachezaji ambao wanaweza kuanza na wale wanaoingia kubadilisha mchezo.
Amesema mechi wanazocheza ni ngumu na zipo karibu sana, kwa hiyo mabadiliko hayo yatawasaidia kutunza ubora wa wachezaji.
“Kuna ule wasiwasi ambao kocha yeyote anaweza kuwa nao anapokuwa na kikosi ambacho hana uhakika wa kupata matokeo, ila kwangu ni tofauti.
“Timu yetu sasa ina sura mbili, kuna wale ambao wanacheza kikosi cha kwanza na wengine wanaanzia benchi, wote wana uwezo wa kuubadilisha mchezo.
“Mpinzani yeyote sasa ana hofu ya kukutana na Simba kwa sababu wanaoingia ni wakali kama waliotoka, kwa hiyo hakuna nafasi ya kupenyeza mashambulizi,” amesema Barker.
Kocha huyo raia wa Afrika Kusini, ameongeza: “Nitakuwa mchoyo nisipowapongeza viongozi wangu kwa nguvu waliyoiongeza dirisha dogo, imezaa matunda sana, hivyo malengo yetu yapo palepale.”
Katika mechi iliyopita dhidi ya Singida Black Stars, Elie Mpanzu alifunga bao la pili dakika ya 84 lililoipa ushindi Simba wa 2-1. Kabla ya hapo, Anicet Oura alianza kuifungia Simba dakika ya 6, kabla ya Ndumumwe Mossi kuisawazishia Singida.
Simba imecheza mechi 12 za Ligi Kuu Bara ikiwa nafasi ya nne ikikusanya pointi 27 baada ya kupoteza moja, sare tatu na kushinda nane.