Dar es Salaam. Ijumaa Machi 13, 2026 Mahakama Kuu Dar es Salaam ilitoa uamuzi wa shauri la kupinga Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, ambapo iliihalalisha tume hiyo.
Katika makala haya tunakuletea kwa undani kuhusu uamuzi huo kwa kuangazia malalamiko ya msingi katika shauri hilo, uchambuzi wa Mahakama wa hoja na msimamo iliyoufikia na hatimaye mtizamo wa walalamikaji.
“Kwa hiyo, kinyume na mtazamo wa waombaji, ni hitimisho la Mahakama hii kwamba, kwa kuzingatia uzoefu mkubwa na upeo mpana wa makamishna katika nyanja mbalimbali za utumishi wa umma, mtu mwenye busara angepongeza uteuzi wa makamishna hao.
“Kwa kuzingatia yote yaliyoelezwa hapo juu, ninabaini kwamba, madai ya waombaji ni dhana na mawazo tu kuliko kuwa uhalisia. Kwa kumalizia, ninatupilia mbali maombi haya kwa kukosa msingi, na kwa kuwa hili ni suala la masilahi ya umma, sitoi amri yoyote kuhusu gharama.”
Hivyo ndivyo Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam ilivyohitimisha uamuzi wake katika shauri la kupinga uamuzi wa Rais wa uundaji tume aliyoiita Tume ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 na uteuzi wa makamishna wake.
Uamuzi huo umetolewa na Jaji Awamu Mbagwa aliyesikiliza shauri hilo, ambaye alifikia hitimisho baada ya kuchambua madai ya wadai na hoja za pande zote huku akizipima katika mzani wa sheria husika na kesi mbalimbali za rejea.
Hata hivyo, wadai na mawakili wao hawakuridhishwa na uamuzi huo, namna Mahakama ilivyochambua na kujibu madai na hoja zao huku wakidai kuwa, kuna hoja zao za msingi kuwa, Mahakama haikuzijibu kabisa, hivyo wameamua kukata rufaa Mahakama ya Rufani.
Ili kupata picha kamili ya uamuzi huo, msingi wa Mahakama kufikia hitimisho hilo na sababu za wadai kuukataa, ni muhimu kwanza turejea madai ya wadai, sababu na hoja za kuipinga tume hiyo na za Mahakama zilizoifikisha katika hitimisho hilo.
Oktoba 29, siku ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 nchini kuliibuka vurugu zilizosababisha uharibifu wa miundombinu, mali za umma, vifo na majeruhi, kufuatia maandamano ya kupinga uchaguzi huo.
Novemba 18, 2025 Rais Samia Suluhu Hassan aliunda tume kuchunguza matukio hayo, inayoongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania mstaafu, Mohamed Chande, akiwa mwenyekiti, inayojulikana kama Tume ya Jaji Chande au Tume ya Matukio ya Oktoba 29.
Pia, Rais Samia aliwateua wajumbe au makamishna tisa wa tume hiyo.
Wajumbe hao ambao pia ndio msingi wa shauri hilo ni Jaji Mkuu mstaafu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma, Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu, Balozi Ombeni Sefue, Radhia Msuya, Balozi Paul Meela na Balozi George Kahema Madafa.
Wengine ni Mkuu wa Jeshi la Polisi mstaafu (IGP), Said Mwema, Balozi David Kapya, aliyewahi kuwa Katibu Mkuu mstaafu wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Africa (SADC) na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa mstaafu, Dk Stergomena Tax.
Rais Samia aliizindua tume hiyo Novemba 20, 2025, huku akiipa miezi mitatu kukamilisha jukumu hilo.
Uundwaji wa Tume hiyo pamoja na uteuzi wa Makamishna wake ulichapishwa katika Gazeti la Serikali (GN) la 20 Novemba 2025.
Hata hivyo, wanaharakati na watetezi wa haki za binadamu, Rosemary Mwakitwange na mawakili wawili Edward Heche na Deogratius Mahinyila, walifungua shauri la maombi ya mapitio ya Mahakama dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na wenzake, baada ya kupata ridhaa ya mahakama hiyo.
Wajibu maombi wengine katika shauri hilo la maombi ya mapitio ya Mahakama namba 32537 la mwaka 2025 ni mwenyekiti na wajumbe hao wa tume hiyo isipokuwa Balozi Madafa na Chama cha Sheria Tanganyika (TLS).
Kwa mujibu wa waombaji, TLS iliundwa mwaka 1954 kwa Sheria ya Bunge, majukumu yake ya msingi yakiwa ni kulinda na kusaidia umma kupata haki na huduma za kisheria katika masuala yote yanayohusu sheria.
Waliipinga tume kwa msingi kwamba, uamuzi wa kuunda Tume hiyo na kuteua makamishna wake haukuwa halali, haukuwa wa busara, ulifanywa kwa nia mbaya, ulikuwa na upendeleo na ni matumizi mabaya ya mamlaka.
Katika shauri hilo waombaji hao waliowakilishwa na mawakili Mpale Mpoki, Hekima Mwasipu na Jebra Kambole walioiomba Mahakama hiyo itoe amri za kufuta na zuio la uamuzi wa Rais wa uteuzi wa wajumbe wa tume hiyo.
Katika hati ya maombi walidai kuwa, tume hiyo haikukidhi vigezo vya kisheria kwa kuwa uundwaji na uteuzi wa wajumbe wake ulifanywa kwa nia ovu kinyume cha kanuni ya haki asili ya mtu kutokuwa hakimu wa kesi yake mwenyewe.
Walifafanua hoja hiyo kuwa kwanza, mamlaka ya uteuzi ni mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi, chama tawala, kilichoshiriki na kushinda uchaguzi uliosababisha ghasia wakati na baada ya uchaguzi, hivyo kina masilahi katika uchaguzi huo na tume hiyo.
Pia, walidai kuwa, mjumbe Tax ni mtuhumiwa kwa kuwa alikuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa wakati ghasia za uchaguzi zilipotokea, alihusika kwa namna moja au nyingine chini ya wizara yake.
Vilevile walidai kuwa, majaji wakuu wastaafu hawawezi kuchunguza kwa haki vurugu hizo kwa kuwa, baadhi ya mali zilizoharibiwa ni za Mahakama waliyoiongoza; na IGP mstaafu hawezi kumchunguza kwa haki, kwa kuwa, IGP aliyepo anaweza kuwa miongoni mwa watuhumiwa.
Waliongeza kuwa, Amiri Jeshi Mkuu (Rais) katika tarehe tofauti alitoa maagizo kwa Polisi na Jeshi kujiandaa kwa ghasia za wakati na baada ya uchaguzi.
Katika hoja nyingine wanadai kuwa, uundaji wa tume hiyo umekiuka masharti ya Sheria ya Tume ya Uchunguzi, Sura 32 Marejeo 2023.
Walidai kuwa, hakuna ufafanuzi wa madhumuni yake yaliyo wazi kama kifungu hicho kinavyoielekeza mamlaka ya uteuzi bali yanategemea hisia tu, kinyume na misingi ya Katiba, utawala bora na utaratibu sahihi wa haki.
Pia, walidai maneno yaliyotumika, ‘uchunguzi wa matukio ya uvunjifu wa amani’ yanapunguza na kudharau vifo, watu waliopotea, miili iliyopotea, majeraha na athari kubwa kwa umma kwa jumla.
Hoja nyingine walidai kuwa tume hiyo si huru.
Walifafanua kuwa, haikujumuisha wajumbe kutoka vyama huru vya kitaaluma kama TLS, Chama cha Madaktari, mashirika ya kijamii ya kidini kama Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) au wadau wengine huru wasio na mgongano wa masilahi, kuepuka upendeleo kwa mamlaka ya uteuzi.
Badala yake walidai kuwa, wajumbe wote ni watumishi wa umma waliostaafu, waliokuwa na nafasi za kuteuliwa na Rais, waliokula kiapo cha siri kwa Rais, ambacho hakijafutwa wakati wa kustaafu au hadi tarehe ya uteuzi kama wajumbe wa tume inayopingwa.
Hivyo, walidai kuwa wajumbe hao hawawezi kuchunguza mamlaka ya uteuzi wao.
Maombi ya waombaji yaliungwa mkono na kiapo na maelezo yaliyotolewa kwa pamoja na waombaji.
Baada ya kuona msingi wa hoja za waombaji kuipinga tume hiyo, sehemu ijayo tutaona kile wajibu maombi wote walichokijibu na hoja za mawakili wakati wa usikilizwaji shauri hilo.