KOCHA Mkuu wa JKT Queens, Abdallah Kessy amesema anapanga kucheza mechi za kirafiki zisizopungua tatu kabla ya kurejea kwa ligi ili kuipima timu na kujua changamoto.
Kessy alisema maandalizi hayo ni muhimu kwa kikosi hicho baada ya mapumziko ya ligi na michezo ya kirafiki itampa picha halisi ya kiwango cha wachezaji wake kabla ya kurejea tena.
“Kipindi hiki tunatafuta mechi za kirafiki zisizopungua tatu kabla ya ligi kurejea ili niweze kufahamu changamoto za timu na maeneo ambayo tunapaswa kuyafanyia kazi,” alisema Kessy.
Aliongeza mechi hizo zitasaidia kuwapa wachezaji nafasi ya kurejea kwenye viwango vyao pamoja na kuongeza utimamu wa mwili kabla ya kuingia kwenye ratiba ngumu ya ligi.
“Tunataka wachezaji wapate dakika za kutosha uwanjani. Hii itatusaidia kurekebisha makosa na kujiandaa vizuri zaidi kwa michezo ya ligi,” alisema.
Aliongeza baadhi ya wachezaji waliokuwepo kwenye majukumu ya timu ya taifa wamejiunga na kambi ya timu hiyo.
“Kikubwa kwetu ni kuona timu inakuwa imara zaidi ndiyo maana tutacheza na timu za ligi ambazo tunakutana nazo mara nyingi.”
