Bwana Yesu asifiwe! Karibu kwenye tafakari ya Neno la Mungu siku ya leo Jumapili ambapo tumepewa somo linalosema ‘Njia za Mungu kujiondoa katika mipaka ya kiroho’. Katika maisha ya mwanadamu kuna mambo mengi yanayoonekana kwa macho, lakini pia kuna mambo mengi yasiyoonekana yanayotawala maisha ya watu.
Moja ya mambo hayo ni mipaka katika ulimwengu wa roho. Mipaka ni vizuizi vinavyoonyesha mwisho wa jambo fulani na kuzuia kitu kisivuke kwenda upande mwingine.
Katika ulimwengu wa roho kuna mipaka ambayo huwekwa ili kuzuia mtu asikue, asiendelee au asipige hatua katika maisha yake. Ndiyo maana mara nyingi tunaona mtu anaanza vizuri katika jambo fulani, lakini baadaye maisha yake yanakwama na kubaki katika kiwango kilekile kwa muda mrefu sana.
Watu wengi hujiuliza kwa nini biashara zao hazikui, kwa nini ndoa hazipatikani, kwa nini kazi haziongezeki, au kwa nini huduma za kiroho hazipanuki. Mara nyingi sababu ya mambo haya huwa ni mipaka iliyowekwa katika ulimwengu wa roho inayosema mtu huyu asivuke kiwango fulani.
Biblia inaonyesha kuwa hata katika uumbaji, Mungu aliweka mipaka kwa vitu mbalimbali. Katika Ayubu 38:11 Mungu anasema, “Utafika mpaka hapa lakini hutapita.” Hii inaonyesha kuwa mipaka ni kanuni inayofanya kazi hata katika mambo ya kiroho na ya asili.
Adui wa maisha ya mwanadamu naye hutumia kanuni hiyo hiyo ya mipaka ili kuzuia maendeleo ya watu. Mara nyingi mipaka hii hupandwa katika mwanzo wa jambo fulani, kama vile mwanzo wa mwaka, mwanzo wa kazi, mwanzo wa biashara au mwanzo wa huduma ya kiroho.
Mathayo 13: 25-26. Katika mfano wa Yesu kuhusu ngano na magugu, tunaona kuwa adui alipanda magugu wakati watu wamelala.
Hii inaonyesha kuwa wakati mwingine mipaka hupandwa bila mtu kujua, lakini baadaye huanza kuonekana pale maisha yanaposhindwa kusonga mbele.
Dalili za uwepo wa mipaka katika maisha zinaweza kuwa nyingi. Kanisa linaweza lisikue, migogoro ikaongezeka, utoaji wa sadaka ukawa dhaifu na watu wakashindwa kusikia sauti ya Mungu. Haya yote yanaweza kuwa ishara kwamba kuna mipaka iliyowekwa kiroho.
Katika maisha binafsi pia dalili zinaweza kuonekana. Mtu anaweza kushindwa kuoa au kuolewa kwa muda mrefu, mimba zikaharibika mara kwa mara, au watoto wakashindwa kufikia mafanikio makubwa katika elimu na kazi. Hali hizi zinaweza kuonyesha kuwa kuna vizuizi vya kiroho vinavyokwamisha maendeleo.
Njia mojawapo inayotumika kuweka mipaka ni maneno. Maneno yana nguvu kubwa sana katika ulimwengu wa roho. Biblia inasema uzima na mauti viko katika uwezo wa ulimi. Maneno yanapotamkwa mara nyingi huweka msingi wa kile kitakachotokea katika maisha ya mtu.
Wakati mwingine mtu anaweza kujitamkia maneno mabaya bila kujua na kujikuta amejiwekea mipaka mwenyewe. Mfano, mtu anaposema hawezi kufanikiwa au hawezi kufanya jambo fulani, maneno hayo yanaweza kuwa kifungo kinachozuia mafanikio yake baadaye.
Njia nyingine inayotumika kuweka mipaka ni maagano. Agano ni makubaliano yanayounganisha watu au vitu viwili kwa kusudi fulani. Maagano yana nguvu kubwa katika ulimwengu wa roho kwa sababu yanaweza kuamua maisha ya mtu yaende kwa kiwango gani.
Watu wengi wanajikuta wameshikiliwa na maagano ya zamani bila kujua. Maagano yanaweza kuwa ya kifamilia, ya kimila, au hata ya mahusiano ya zamani. Maagano hayo yanaweza kuzuia baraka fulani zisitokee mpaka yatakapovunjwa.
Tabia za mtu pia zinaweza kuwa mipaka ya maendeleo.
Tabia kama uvivu, wivu, uzinzi, ugomvi na ulevi huweza kuzuia mtu kupanda katika viwango vya juu vya maisha. Tabia mbaya humvuta mtu karibu na mazingira mabaya ambayo yanaharibu mustakabali wake.
Aidha, uchawi na uganga ni njia nyingine zinazotumiwa kuweka mipaka katika maisha ya watu. Watu wanaweza kulogwa au kufungiwa kiroho ili maisha yao yasisonge mbele. Hali hii huathiri biashara, huduma, familia na hata afya.
Habari njema ni kwamba mipaka yote inaweza kuondolewa kupitia nguvu ya Mungu. Hatua ya kwanza ni kumrudia Mungu kwa toba ya kweli na maisha ya wokovu. Wokovu humpa mtu mamlaka ya kushinda nguvu za giza.
Pili, mtu anahitaji kupata maarifa sahihi kuhusu tatizo linalomzuia. Maarifa humsaidia mtu kuelewa chanzo cha tatizo na kuanza kupambana nalo kwa njia sahihi ya kiroho.
Tatu, ni muhimu kufanya maombi ya nguvu kwa uongozi wa Roho Mtakatifu. Maombi ya mamlaka huvunja minyororo ya kiroho na kuondoa vizuizi vilivyowekwa na adui.
Jambo la nne ni sadaka inayotolewa kwa imani na moyo wa kumheshimu Mungu inaweza kufungua milango iliyofungwa. Mungu ana uwezo wa kuondoa mipaka yote na kumruhusu mtu kuvuka viwango ambavyo hapo awali vilionekana haviwezekani. Iwe ni sehemu kazi kwako, kwenye biashara yako unapoona unatumia nguvu kubwa lakini mambo hayaendi, yupo Mungu aliyehai ambaye sikio lake sio zito. Mgeukie kwa moyo wa unyeyekevu, ninao uhakika atakusaidia kwa sababu neno lake ni kweli na amina. Mungu akubariki sana.
