Na: Mwandishi Wetu
Wanachama wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), tawi la China (Diaspora), limeandaa Kongamano la Siku ya Kimataifa ya Wanawake 2026 kwa njia ya mtandao (Google Meeting) ili kujadili masuala mbalimbali ya kimaendeleo yamuhusuyo mwanamke.
Kongamano hilo linatarajiwa kufanyika Machi 15, 2026, majira ya saa tisa kamili alasiri hadi saa kumi na mbili kamili jioni. Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa (MCC) na Mbunge wa Viti Maalum, Mary Chatanda, anatarajiwa kushiriki Kongamano hilo akiwa Mgeni Rasmi.
“Nimefurahi kupata mwaliko huu ambao kama wanawake tutajadili masuala mbalimbali ya kumuinua mwanamke kimaendeleo na changamoto zinazomkabili mwanamke kama tunavyojua mwanamke ni nguzo na kiungo muhimu katika maendeleo kuanzia ngazi ya familia hadi Taifa. Kwa kweli tunajivunia kuona mwanamke mwenzetu, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, akionyesha uwezo mkubwa wa kiuongozi,” amesema Chatanda.
Viongozi wengine watakaoshiriki Kongamano hilo la Wanawake ni pamoja na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) anayeshughulikia Masuala ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa – SUKI, Rabia Hamid, Mbunge wa Viti Maalum Vijana, Timida Fyandomo, Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Rebeca Nsemwa na Mkuu wa wilaya ya Lindi, Victoria Mwanziva.
Wanachama wa CCM waishio nchini China wameandaa kongamano hilo ikiwa ni njia ya kuenzi mchango wa mwanamke katika maendeleo ya nchi. Ikumbukwe Siku ya Kimataifa ya Wanawake huadhimishwa kila mwaka ifikapo Tarehe 08 Machi, ambapo kwa mwaka huu 2026, maadhimisho hayo yamechagizwa na kaulimbiu isemayo ” Haki na Usawa kwa Wanawake na Wasichana: Msingi Jumuishi Kufikia Dira 2050.”