Dar es Salaam. Mvua kubwa zinazoendelea katika maeneo mbalimbali nchini zimeongeza hatari ya mafuriko, uharibifu wa miundombinu na changamoto za kiafya, huku wataalamu wakionya kuwa mabadiliko ya tabianchi na ukuaji wa kasi wa miji vinafanya matukio hayo kuwa ya mara kwa mara.
Mvua hizo zilizoanza mwishoni mwa mwezi uliopita ni sehemu ya mwanzo wa msimu wa mvua za masika unaotarajiwa kuendelea kuanzia Machi hadi Mei. Hata hivyo, mamlaka husika zinasema mwenendo wa sasa wa hali ya hewa unaashiria kuwa mvua zitakuwa kubwa na kudumu kwa muda mrefu kuliko kawaida.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeonya kuwa kiwango cha mvua kinaweza kuongezeka katika siku zijazo, hali inayoweza kuongeza uwezekano wa mafuriko katika baadhi ya mikoa.
Maeneo ya ukanda wa pwani, ikiwemo mikoa ya Lindi, Mtwara, Pwani na visiwa vya Mafia, yametajwa kuwa katika hatari kubwa ya kukumbwa na athari za mvua hizo, ikiwemo usumbufu wa usafiri na shughuli za baharini.
Utabiri wa awali pia ulionesha mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro na Tanga inaweza kupata mvua za kiwango cha kawaida hadi juu ya wastani, jambo linaloweza kuongeza hatari ya mafuriko pamoja na magonjwa ya mlipuko yanayosababishwa na mvua.
Akizungumza na Gazeti la The Citizen leo Jumapili, Machi 15, 2026, Mkurugenzi wa Mazingira katika Ofisi ya Makamu wa Rais, Kanizio Manyika, amesema tafiti za kisayansi zinaonesha kuwa mabadiliko ya tabianchi yanaongeza ukubwa wa matukio ya hali mbaya ya hewa.
Amesema kuongezeka kwa joto duniani kunafanya anga kuwa na uwezo mkubwa wa kubeba unyevunyevu, hali inayoongeza uwezekano wa kunyesha mvua nyingi kwa muda mfupi na kusababisha mafuriko.
Aidha, amesema hatari ya mafuriko inaongezwa na shughuli za kibinadamu, zikiwamo upanuzi wa haraka wa miji, ujenzi wa makazi katika mabonde ya mito na njia za kupitisha maji, uharibifu wa misitu na maeneo oevu pamoja na miundombinu isiyoandaliwa kuhimili mvua kubwa.
Kwa mujibu wa Manyika, miji iliyoko katika maeneo ya chini kama Dar es Salaam imeendelea kuwa katika hatari kubwa zaidi, kwa sababu mvua kubwa mara nyingi husababisha usumbufu katika usafiri wa barabarani, uharibifu wa miundombinu na kuongezeka kwa hatari ya milipuko ya magonjwa pale mifumo ya mifereji inapoziba na maji kufurika.
Kaskazini mwa Tanzania, mvua zilizonyesha hivi karibuni zimesababisha mafuriko katika baadhi ya barabara zinazoingia kwenye mfumo wa ikolojia wa Serengeti, hali iliyosababisha shughuli za utalii kusimama kwa muda huku matengenezo ya dharura yakifanyika kurejesha miundombinu hiyo.
Sekta ya kilimo pia inatajwa kuwa miongoni mwa zilizo katika hatari, kwani mafuriko yanaweza kusababisha mmomonyoko wa udongo, kuharibu mazao na kuchelewesha shughuli za upandaji.
Hata hivyo, imeelezwa kuwa wakati mvua zikiendelea, Serikali imeanza kuchukua hatua mbalimbali za kupunguza athari zake.
Dk Manyika amesema mifumo ya tahadhari ya mapema imeimarishwa kupitia TMA, huku timu za usimamizi wa maafa zikishirikiana kuratibu uhamishaji wa wananchi kutoka maeneo yenye hatari ya mafuriko.
Pia, makazi ya muda na misaada ya kibinadamu, ikiwemo chakula, huduma za afya na malazi, vinaandaliwa kwa watu watakaoathiriwa.
“Serikali imeanza kujenga miundombinu inayoweza kuhimili mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuwekeza katika miradi ya kudhibiti mafuriko, kuboresha mifereji ya maji mijini na kulinda misitu na maeneo oevu yanayosaidia kudhibiti mtiririko wa maji,” amesema.
Wataalamu wa hali ya hewa wanaonya kuwa mvua zinazoendelea huenda ni mwanzo tu wa msimu wa masika unaotarajiwa kufikia kilele chake mwezi Aprili.
