Unguja. Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo Taifa, Othman Masoud Othman, amewaondoa wasiwasi wanachama na wananchi, akiwataka wawe watulivu kwa kuwa mazungumzo ya kuleta suluhu ya kisiasa Zanzibar yanaendelea vizuri.
Kauli ya Othman inakuja wakati ambapo chama chake kiko katikati ya mazungumzo na CCM na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuhusu mustakabali wa siasa na uamuzi wa kuingia katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).
Pia ametoa kauli hiyo ikiwa imepita zaidi ya miezi minne tangu ACT-Wazalendo kushindwa kuingia SUK, huku kamati maalumu inayowahusisha viongozi wastaafu wa Serikali ya Zanzibar ikiundwa kuutafuta mwafaka.
Wakati wakiingia kwenye mazungumzo hayo, ACT-Wazalendo kilichukua hatua nyingine, ikiwemo kufungua kesi kwa baadhi ya majimbo ya uwakilishi Unguja na Pemba, wakipinga michakato iliyofanyika katika uchaguzi huo na kuwapata washindi.
Hata hivyo, kesi hizo hazikufaulu baada ya zote kutupiliwa mbali na Mahakama Kuu ya Zanzibar kutokana na makosa ya kisheria.
Othman ametoa kauli hiyo Machi 14, 2026, alipowafutarusha wanachama na wananchi katika Mkoa wa Mjini Magharibi, visiwani Zanzibar.
Amesema wananchi wanapaswa kuwa na subira na kujenga matumaini mema kuhusu mazungumzo yanayoendelea kati ya pande hizo.
“Tunakuombeni mzidishe subra na matumaini ya kheri, tulipofikia ni pazuri na tunaendelea vyema,” amesema Othman.
Othman, aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais katika kipindi cha utawala wa Rais Mwinyi awamu ya kwanza, ameendelea kusisitiza kwa waumini na wananchi kwa ujumla, haja ya kuiombea dua nchi ili irudi katika misingi ya ustaarabu, umoja, na uungwana kama ilivyokuwa hapo awali.
Amesema kwa wanaoifahamu nchi hiyo, wanaona tofauti kubwa iliyopo sasa katika mnasaba wa mabadiliko ya haki. Amehimiza wajibu wa umma kushikamana kwa ajili ya kuleta mageuzi na kurudisha upya mwenendo unaozingatia haki hizo.
“Ni wajibu wetu sasa tuungane sote ili kuirudisha nchi katika misingi yake ya asili inayofanana na uhalisia wake,” amesema Othman.
Mazungumzo hayo kwa ACT-Wazalendo yanaongozwa na Othman mwenyewe, huku upande wa CCM ukisimamiwa na marais wastaafu—Amani Abeid Karume na Dk Ali Mohamed Shein.
Iwapo mazungumzo hayo yatafikia mwafaka, ACT-Wazalendo kwa mara nyingine kitakuwa sehemu ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Kitakachosubiriwa ni kuona ni nani atakayeteuliwa na chama hicho kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais, huku wengine watateuliwa kuwa mawaziri katika nafasi nne zilizoachwa wazi.
