Serikali kuendelea kuimarisha miundombinu ya elimu

 

-Kamati yaridhishwa na ujenzi Chuo kikuu Mzumbe kampasi ya Tanga

Na Mashaka Mhando, Mkinga

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya elimu ya juu kupitia miradi ya kimkakati ikiwemo ule wa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), ili kuchochea utafiti na ubunifu utakaosaidia maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Prof. Mkenda ametoa kauli hiyo wilayani Mkinga wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Michezo na Utamaduni ilipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Kampasi ya Tanga ya Chuo Kikuu Mzumbe.

Alisema serikali itaendelea kuboresha lakini pia alisema kuwa atahakikisha anavuta wawekezaji wengine binafsi kujenga taasisi za elimu katika eneo hilo.

Alisema Wizara itahamasisha taasisi nyingine za elimu na sekta binafsi kuwekeza Mkinga ili kukuza dhana ya mji wa kitaaluma. Alibainisha kuwa mkoa wa Tanga utapewa kipaumbele kwa Chuo hicho kufundisha kozi za kimkakati ikiwemo uchumi wa Buluu (Blue Economy) Madini na Uvuvi ili kuendana na fursa za mkoa huo.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha, ameiambia kamati hiyo kuwa ujenzi wa miundombinu hiyo umefikia asilimia 82, ukijumuisha jengo la taaluma, kituo cha afya, mabweni ya wanafunzi, mkahawa, nyumba za wafanyakazi pamoja na mifumo ya maji safi na taka.

Akijibu maswali ya wabunge waliotaka kujua mkandarasi kuongezewa muda Profesa Mwegoha alisema unatarajiwa kukabidhiwa mwezi Mei mwaka huu na utahudumia wanafunzi 1,500 na mradi una thamani ya Shilingi Bilioni 16.

“Eneo hili lina ekari 300 na ujenzi unazingatia Master Plan ya kisasa. Changamoto kubwa iliyotuchelewesha ni mazingira ya kijiografia ikiwemo miamba na ubovu wa barabara wakati wa mvua, lakini mkandarasi Dimetoclasa Real Hope Ltd yupo asilimia 82 ya utekelezaji,” alisema Prof. Mwigoha.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Husna Sekiboko, amesisitiza umuhimu wa mradi huo kukamilika kwa wakati kwa mujibu wa mkataba, huku akibainisha kuwa taarifa za ziara hiyo zitasaidia katika maandalizi ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

“Tumeridhishwa na hatua iliyofikiwa na tunatarajia kazi zote zikamilike kwa wakati ili mradi huu uanze kutoa tija iliyokusudiwa na Serikali katika kuimarisha uwekezaji wa elimu ya juu,” amesema Sekiboko.

Kampasi hiyo ya Chuo Kikuu Mzumbe inajengwa katika Kijiji cha Pangarawe, Kata ya Gombero wilayani Mkinga, mwenyekiti wa Kamati alisema kuwa Wizara ya Elimu iweke wazi mahitaji ya kifedha ili kukamilisha miundombinu wezeshi.

Ziara hiyo ya kikazi ililenga kukagua utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2025/2026 na utekelezaji wa Ilani ya CCM.

Mwenyekiti wa Kamati, Mhe. Husna Sekiboko, alipongeza thamani ya fedha (Value for Money) inayoonekana katika majengo hayo, lakini akaonya kuhusu kusuasua kwa huduma za kijamii. “Haiwezekani mwanafunzi wa Chuo Kikuu abebe ndoo kutafuta maji au barabara ishindwe kupitika. Tunataka Wizara iwe wazi katika mtiririko wa fedha za bajeti ya 2026/2027 ili tumalize kero ya barabara ya kilomita 16 kutoka Mabokweni na umeme wa uhakika,” alisisitiza Mhe. Sekiboko.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mkinga, Mhe. Jumaa Kasinya, alitangaza neema kwa wabunge na wawekezaji kwa kusema kuwa Halmashauri imetenga ekari 500 kwa ajili ya “Academic City” na amewahamasisha wajumbe wa Kamati hiyo kufika na wao wawe sehemu ya uwekezaji katika eneo hilo.

Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, Mhe. Gilbert Kalima, aliongeza kuwa kufuatia agizo la Waziri Mkuu, TARURA tayari wamefanya tathmini ya ujenzi wa barabara za lami ndani ya chuo hicho, ambapo aliomba ziongezwe hadi kilomita tano ili kuongeza hadhi ya kampasi hiyo.

Wajumbe wa Kamati, akiwemo Baraka Mwamengo, Asha Feruzi, na Yumna Mmanga Omar, walipongeza uamuzi wa Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuweka chuo hicho Mkinga, wakisisitiza kuwa maboresho ya barabara  za ndani zitazamwe ikiwemo kusimamia mkandarasi aweze kumaliza Chuo hicho kwa wakati alioongezewa.

Viongozi wa Mkoa wa Tanga na Wilaya ya Mkinga waliohusika katika ziara hiyo wameeleza kuwa kukamilika kwa kampasi hiyo kutachochea fursa za ajira na kuvutia uwekezaji katika maeneo ya jirani, jambo litakaloinua uchumi wa wananchi wa ukanda huo.