Serikali kujenga gati mpya kilipo Chuo cha Bandari

Dar es Salaam. Serikali imekusudia kukihamisha Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI)  na kutumia eneo hilo kwa ajili ya kujenga gati ikiwa ni moja ya hatua za kupanua Bandari ya Dar es Salaam.

Kuhamishwa kwa chuo hicho, kunalenga kukipeleka katika eneo kubwa zaidi la Kimbiji lililopo Kigamboni jijini Dar es Salaam kutoka katika eneo finyu walilopo sasa.

Hayo yamesemwa leo Jumapili Machi 15, 2026 baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuweka bayana kuwa vyuo vingi vilivyo chini ya Wizara ya Uchukuzi kikiwamo DMI vinafanya kazi katika mazingira yasiyoridhisha na yanahitaji maboresho makubwa ili kuendana na mahitaji ya sasa ya elimu ya kitaaluma pamoja na maendeleo ya sekta ya uchukuzi nchini.

Azma hiyo imewekwa wazi baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu iliyofanya ziara katika Bandari ya Dar es Salaam sambamba na chuo hicho.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Selemani Kakoso amesema baadhi ya vyuo vilivyo chini ya Wizara ya Uchukuzi vinafanya kazi katika maeneo finyu yasiyowapa watumishi na wanafunzi nafasi ya kufanya shughuli zao kwa uhuru.

Amesema ni muhimu taasisi hizo kuhamishiwa katika maeneo mapana yatakayowezesha utoaji wa mafunzo kwa ufanisi zaidi.

“Ukienda katika baadhi ya vyuo hivi utashangaa hali ilivyo. Kwa mfano chuo cha mamlaka ya anga kinafanya kazi katika mazingira ambayo hayavutii na hayalingani na hadhi ya taasisi hiyo,” amesema Kakoso.

Amesema hata katika karakana za Shirika la Reli kuna juhudi za kiufundi kama kuunganisha vifaa vya treni na mipango ya kujenga mabehewa, lakini bado maeneo hayo hayajapewa kipaumbele cha kutosha katika maboresho ya miundombinu.

Kakoso amesisitiza kuwa Serikali inapaswa kuwekeza zaidi katika kuboresha vyuo vilivyo chini ya Wizara ya Uchukuzi ili viweze kutoa elimu bora na kuvutia wanafunzi wengi zaidi, wakiwamo kutoka nje ya nchi.

“Baadhi ya vyuo vinahitaji uwekezaji mkubwa wa miundombinu. Kwa mfano chuo hiki cha bandari kinahitaji takribani Sh20 bilioni kwa ajili ya maboresho ya majengo na mazingira ya kujifunzia,” amesema.

Ameongeza kuwa endapo vyuo hivyo vitawezeshwa kwa mtaji wa awali, vina uwezo wa kujiendesha na hata kupata mapato kupitia huduma na mafunzo wanayotoa.

Akijibu hoja hiyo kwa upande wa Chuo cha DMI, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema Serikali inafahamu changamoto zilizopo na umuhimu wake katika sekta ya bandari na uchukuzi kwa ujumla.

Amesema tayari uamuzi umefanyika ambapo Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) itachukua eneo la sasa la chuo hicho ili kujenga gati jipya la kuhudumia mizigo, huku chuo kikihamishiwa katika eneo la Kimbiji, Kigamboni, ambako kitajengwa upya kwa miundombinu ya kisasa.

“Eneo la sasa litatumika kwa ajili ya ujenzi wa gati jipya la bandari. Hatua hii inalenga kuongeza uwezo wa bandari na kukuza shughuli za uchukuzi na biashara nchini,” amesema Mbarawa.

Naye Mkuu wa Chuo cha Bandari, Profesa Tumaini Gurumo amesema katika mwaka wa fedha wa 2025/26 chuo hicho kimetengewa Sh1.09 bilioni kwa ajili ya kuboresha mazingira ya ufundishaji na miundombinu.

Amesema kati ya fedha hizo, Sh597.670 milioni zimetengwa kwa ajili ya kuendeleza eneo jipya la chuo lililopo Kimbiji, Kigamboni, Dar es Salaam.

“Eneo hili lina ukubwa wa ekari 13 na litasaidia kupanua shughuli za mafunzo na kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi,” amesema Gurumo.

Kamati hiyo imebaini kuwa licha ya kuwepo kwa baadhi ya vifaa vya kisasa vya kufundishia katika chuo hicho, majengo mengi hayapo katika hali nzuri na hayana uwezo wa kubeba idadi kubwa ya wanafunzi wanaosoma katika taasisi hiyo.