SGR kuanza kutoa mizigo bandarini

Dar es Salaam. Serikali imesema kuanzia mwisho wa mwezi huu, itaanza kutumia Treni ya Kisasa (SGR) kusafirisha mizigo moja kwa moja kutoka bandarini, badala ya kutumia bandari ya Pugu kama ilivyokuwa awali.

Hayo yameelezwa baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kudai kuwa uondoshaji wa mizigo bandarini ni sababu inayofanya ufanisi wa bandari kutoonekana kwa haraka.

Hayo wameelezwa wakati kamati hiyo ilipotembelea Bandari ya Dar es Salaam na kufanya ukaguzi wa shughuli za uendeshaji zinazofanyika baada ya kuikaribisha sekta binafsi.

Ziara hiyo imefanyika wakati TPA imeshuhudia ongezeko la uwezo wa kuhudumia shehena kwa mwaka kutoka tani milioni 17 kabla ya maboresho hadi kufikia tani milioni 50.

Akizungumza baada ya ziara hiyo, leo Machi 15, 2026,  Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema Serikali inatambua kuwa ufanisi wa bandari unategemea sana uwezo wa kuondoa mizigo kwa haraka kupitia reli na barabara.

Amesema Serikali inaendelea kuboresha matumizi ya reli ya kisasa ya SGR na reli ya MGR ili kusafirisha mizigo kutoka bandarini kwenda maeneo mbalimbali nchini na nchi jirani. Amesema wanajenga kituo cha kutoa mizigo kutoka bandarini.

“Kuanzia mwisho wa mwezi Machi mwaka huu, MGR itakuwa ikitoa mzigo bandarini, Tazara itatoka bandarini kwenda Tunduma na Kapiri Mposhi, Zambia, SGR itaanza hapa na kwenda Dodoma,” amesema.

Amesema hiyo ni tofauti na sasa ambapo MGR pekee ndiyo inayotoa mizigo kutoka bandarini, ambayo ufanisi wake si mkubwa, huku mizigo inayobebwa na SGR ikichukuliwa na magari kutoka bandarini hadi Pugu inapakiwa katika treni kwa ajili ya kwenda Dodoma na Kwala.

Amesema hatua hiyo itakwenda sambamba na kuiongezea nguvu treni ya Tanzania kwenda Zambia kutoka zaidi ya kilomita 30 kwa saa hadi zaidi ya kilomita 80, ili iweze kusafirisha mizigo ya Zambia na Tunduma, hali ambayo itasaidia kuongeza ushindani wa Bandari ya Dar es Salaam dhidi ya bandari nyingine katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Kwa mara ya kwanza, SGR ilianza kusafirisha mizigo Aprili mwaka jana, na katika mabehewa 264 yaliyopo, 200 yameundwa kubeba makontena na 64 kubeba mizigo isiyofungwa (shehena kichele).

Awali,  mbunge wa Bukoba Mjini, Wilfred Mtasiwa, amesema licha ya maboresho ya kiufundi yaliyofanyika bandarini, miundombinu ya kusaidia uondoshaji wa mizigo kama barabara bado haijaendana na ongezeko la shughuli za bandari.

Amesema ni muhimu taasisi kama Shirika la Reli Tanzania (TRC) na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kupewa takwimu sahihi za mizigo inayohudumiwa sasa, ili ziweze kupanga namna ya kusaidia kusafirisha mizigo kutoka bandarini kwenda maeneo mbalimbali.

“Ni muhimu kuwa na mipango ya pamoja sambamba na kuboresha vituo vya huduma za pamoja mipakani na kuanzisha mfumo wa malipo ya pamoja ili kuharakisha utoaji wa mizigo,” amesema.

Mbunge wa Sengerema, Hamis Tabasamu, amesema uwepo wa mifumo mingi ya kielektroniki katika taasisi mbalimbali umekuwa kikwazo kikubwa katika uondoshaji wa mizigo bandarini.

Ameeleza kuwa Tanzania ina zaidi ya mifumo 20 ambayo haisomani, jambo linalosababisha ucheleweshaji wa mizigo.

Tabasamu amependekeza kuwepo mifumo michache inayounganishwa, ili kurahisisha utoaji wa mizigo mara tu inapofika bandarini.

“Katika baadhi ya nchi kama Afrika Kusini, mizigo huanza kushughulikiwa kabla haijafika bandarini na haipaswi kukaa zaidi ya saa 24. Tufike huko ili kuongeza ufanisi,” amesema.

Mbunge wa Kilombero, Aboubakar Asenga ameitaka Serikali kuisimamia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ili kuharakisha ujenzi wa bandari kavu katika eneo walilopewa la Kwala kwa ajili ya kuhifadhi mizigo yao.

Amesema hatua hiyo itasaidia kupunguza msongamano wa mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam kwa kuhifadhi mizigo hiyo katika bandari kavu wakati ikisubiri kusafirishwa kwenda nchi husika.

Mbunge Said Hamad amesema, pamoja na mafanikio yaliyofikiwa katika kuboresha utendaji wa bandari, bado kuna changamoto ya udokozi wa baadhi ya bidhaa.

Ameitaka Serikali kuimarisha mifumo ya ulinzi na kuongeza ufanisi ili kuvutia magari mengi zaidi ya mizigo kutoka nchi jirani kupita katika bandari za Tanzania.

“Lengo linapaswa kuwa kuongeza idadi ya magari yanayopita nchini kutoka asilimia 60 hadi kufikia asilimia 100,” amesema.

Mbunge wa Monduli, Isaac Joseph, amehoji sababu ya kuwepo kwa magari mengi yaliyopaki bandarini wakati utoaji wa magari unaelezwa kuwa umeongezeka. Amesema matarajio ni kuona maegesho yanapungua kutokana na maboresho ya mifumo na miundombinu.

“Mapato yanapoongezeka ni muhimu kuweka mkakati mzuri wa kuwekeza katika miradi ya kuboresha bandari ili kuongeza ufanisi katika uondoshaji wa mizigo,” amesema.

Akijibu uwepo wa magari bandarini, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa, amesema sababu ya kuwepo kwa magari mengi bandarini ni kwamba meli zinapofika hupakua mizigo kwanza kabla ya kukamilika kwa taratibu nyingine kama uhakiki na ulipaji wa kodi.

Ameeleza kuwa magari mengi hupelekwa katika bandari binafsi za magari kusubiri kukaguliwa na kulipiwa kodi kabla ya kutolewa.

“Tunaendelea kuboresha mifumo na kushirikiana na waendeshaji binafsi wa bandari ili kuongeza ufanisi katika uondoshaji wa mizigo, na mifumo yote hivi sasa inasomana,” amesema.

Mmoja wa wafanyabiashara na mwingizaji wa bidhaa kutoka nje, Laitus Samson, amesema hali hiyo itarahisisha upataji wa mizigo kwa wafanyabiashara wote na kupunguza malalamiko ya wateja.

“Mizigo ya nje ya Dar es Salaam ikitolewa kwa urahisi, ile ya Dar es Salaam inayobaki inakuwa rahisi kuipata tofauti na mizigo yote kuwa sehemu moja,” amesema.