Dar es Salaam. Kumekuwa na sintofahamu kubwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu hatima ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, huku madai yasiyothibitishwa yakisambaa, yakidai kuwa huenda kiongozi huyo amejeruhiwa, amejificha, au ameuawa.
Katika siku za hivi karibuni, machapisho mengi kwenye majukwaa mbalimbali ya kijamii yamekuwa yakidai kuwa Netanyahu hajulikani alipo, hali iliyozua maswali mengi miongoni mwa watumiaji wa mtandao duniani.
Taarifa hizo zilianza kusambaa kwa kasi kupitia majukwaa ya X, Telegram, na WhatsApp, zikidai kuwa Netanyahu ameshambuliwa katika shambulio la kushtukiza dhidi ya makazi yake au msafara wake.
Baadhi ya machapisho hayo yameenda mbali zaidi kwa kudai kuwa kiongozi huyo huenda ameuawa katika mazingira ambayo bado hayajawekwa wazi.
Hata hivyo, hadi sasa hakuna tamko rasmi kutoka Serikali ya Israel, jeshi la nchi hiyo, au ofisi ya Waziri Mkuu lililothibitisha madai hayo.
Uvumi huo unakuja ikiwa ni wiki mbili tangu kuanza kwa vita, kufuatia kifo cha kiongozi mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, kilichotokea Februari 28, 2026, kufuatia shambulizi la pamoja la Marekani na Israel.
Tukio hilo liliibua mfululizo wa mashambulizi ya makombora kutoka Tehran dhidi ya Israel na mataifa mengine ya Ghuba, ambayo Marekani imetajwa kuwa na kambi za kijeshi.
Alipoonekana mara ya mwisho
Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari vya kimataifa, kiongozi huyo alionekana hadharani mara ya mwisho Machi 2, 2026, akitembelea eneo lililoshambuliwa na Iran karibu na mji wa Jerusalem na kutoa hotuba kuhusu operesheni ya kijeshi ya Israel.
Vilevile, Machi 3, 2026, alihudhuria mikutano ya usalama na viongozi wa jeshi mjini Tel Aviv na kushiriki shughuli rasmi za serikali.
Baada ya hapo, kulikuwa na ukimya wa siku kadhaa bila kuonekana hadharani, jambo lililochochea uvumi kwenye mitandao ya kijamii kwamba huenda amejeruhiwa au kuuawa.
Hata hivyo, Serikali ya Israel imesema madai hayo ni “fake news” na imesisitiza kuwa Netanyahu bado yuko hai.
Uvumi huo umeongezeka baada ya video iliyosambaa mtandaoni kudaiwa kuwa ya AI au iliyohaririwa, jambo lililochochea mijadala mikubwa mtandaoni.
Wachambuzi wa siasa za kimataifa wamesema taarifa za aina hiyo mara nyingi huibuka wakati wa mvutano wa kisiasa au kijeshi, na hutumiwa na baadhi ya watu au makundi kusambaza propaganda au kupotosha umma.
Kwa upande mwingine, baadhi ya watumiaji wa mtandao wamekuwa wakitaka uwazi zaidi kuhusu ratiba na shughuli za kiongozi huyo, wakisema ukimya wa muda mrefu kutoka kwa vyanzo rasmi umeongeza mashaka na kuzalisha uvumi.
Akizungumza na Mwananchi Digital kwa njia ya simu, mchambuzi wa siasa za kimataifa Abdallah Kanju amesema: “Ikumbukwe siku ya kwanza ya mashambulizi ya Israel na Marekani walifanikiwa kumuua kiongozi mkuu wa Iran, na sasa kuna uvumi Netanyahu haonekani. Baada ya watu kuhoji, ofisi ya Waziri Mkuu ikachapisha video ikimuonesha akihutubia, lakini wachambuzi wa teknolojia wameichambua video hiyo na kuona ni AI, hivyo hili linazidisha sintofahamu.”
Amesema kutokana na hilo, baadhi ya watu wamezidi kuwa njia panda kulingana na taarifa hizo, ambapo tena ofisi ya Waziri Mkuu ilichapisha taarifa ikisema taarifa hizo hazjathibitishwa, na baadaye wakaifuta.
“Sasa hivi sura ya vita imeshabadilika, na maoni ya watu wengi yanaonesha Iran imeshashida vita hivi, ijapokuwa wao wanapata madhara. Kama itakua ameuawa, sura ya vita itabadilika; kama vita itaendelea kupanuka au ikaisha, ijapokuwa taarifa rasmi,” amesema.
Hata hivyo, wataalamu wa habari wamesisitiza kuwa katika zama za teknolojia na mitandao ya kijamii, uvumi unaweza kusambaa kwa kasi kubwa kuliko taarifa sahihi.
Hadi sasa, hakuna chombo cha habari cha kimataifa au cha Israel (kama vile Haaretz au Times of Israel) ambacho kimethibitisha madai hayo.
