Sio Ibenge wala Pedro Daresalaam Dabi

LICHA ya kushuka dimbani ikiwa na safu kali ya ushambuliaji inayoundwa na washambuliaji hatari wa Ligi Kuu Bara kwa sasa, Depu na Prince Dube, wenye jumla ya mabao 12, Yanga imeshindwa kuonyesha makali yake mbele ya lango baada ya kutopiga hata shuti moja lililolenga lango la Azam FC katika mchezo uliomalizika kwa suluhu.

Mchezo huo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, umezikutanisha timu hizo zenye ushindani mkubwa, lakini zote zimeshindwa kutumia nafasi zilizopata.

Katika kipindi cha kwanza, timu zote zilianza kwa tahadhari huku zikishambuliana kwa zamu na kutegemea zaidi mashambulizi kupitia maeneo ya pembeni.

Azam FC, licha ya kukosa mshambuliaji wa kati wa asili, ilipiga mashuti matatu ambapo moja lililenga lango, wakati Yanga ilipiga mashuti mawili ambayo yote hayakulenga lango.

Mwanzoni mwa kipindi cha pili, kocha wa Azam FC, Florent Ibenge, alifanya mabadiliko ya mapema akimtoa Ashraf Kibeku na kumuingiza Jean Ngita ili kuongeza nguvu kwenye eneo la ushambuliaji.

Mabadiliko hayo yalimfanya Feisal Salum, aliyekuwa akicheza kama mshambuliaji wa kivuli, kushuka chini zaidi na kucheza nafasi yake ya kawaida ya kiungo mshambuliaji namba 10 ili kusaidia kutengeneza nafasi.

Dakika ya 60, Yanga nayo ilifanya mabadiliko kwa kumtoa Mudathir Yahya na kumuingiza Pacome Zouzoua katika jitihada za kuongeza ubunifu na kasi katika safu ya ushambuliaji.

Hata hivyo, juhudi za timu zote mbili hazikuzaa matunda hadi dakika 90 zinakamilika na kuifanya kila timu kuondoka na pointi moja.

Kwa matokeo hayo, Yanga imeendelea kuongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara kwa kufikisha pointi 36, huku Azam FC ikishika nafasi ya pili ikiwa na pointi 28.

Kikosi cha Azam FC: Aishi Manula, Lusajo Mwaikenda, Pascal Msindo, Yoro Diaby, Yeison Fuentes, James Akaminko, Zidane Sereri, Himdi Mao, Feisal Salum, Iddi Selemani na Ashraf Kibeku.

Kikosi cha Yanga: Djigui Diarra, Israel Mwenda, Mohamed Hussein, Ibrahim Abdulla, Bakari Mwamnyeto, Mudathir Yahya, Maxi Nzengeli, Allan Okello, Laurindo Dilson, Prince Dube na Duke Abuya.