Matatizo mengi tunayokutana nayo katika uhusiano wa kila siku yana mizizi yake katika tofauti za kijinsia.
Ukweli kwamba mpenzi wako ni mwanaume na wewe ni mwanamke, au kinyume chake, unatosha kabisa kuleta tofauti fulani ambazo, zisipoeleweka vizuri, huweza kusababisha misuguano na migongano isiyo ya lazima.
Ni muhimu kufahamu kwamba wanaume na wanawake tumetengenezwa tofauti kimaumbile, kisaikolojia na kihisia, lakini tofauti hizi hazimaanishi kwamba mmoja ametengenezwa kimakosa. Kila mmoja ametengenezwa kwa namna yake, na tofauti hizo ndizo zinapaswa kueleweka na kuheshimiwa.
Jambo la msingi katika uhusiano ni kujifunza kutofautisha kati ya tofauti tulizonazo na matatizo tuliyonayo. Tofauti zetu zinatokana zaidi na asili ya kijinsia; kwamba huyu ni mwanaume na yule ni mwanamke.
Matatizo, kwa upande mwingine, husababishwa na mambo mengi kama malezi na makuzi, mazingira tuliyokulia, aina ya watu tunaoishi nao kwa muda mrefu, historia ya maisha ya nyuma pamoja na uzoefu wa uhusiano wa awali. Changamoto kubwa kwa wengi ni kushindwa kutambua mpaka kati ya tofauti na tatizo.
Wengi hufanya makosa kwa kujaribu kutatua tofauti kana kwamba ni matatizo. Ukweli ni kwamba misuguano inayotokana na tofauti za kijinsia haiwezi kutatuliwa, bali inaweza tu kueleweka na kukubalika.
Kinachotakiwa kufanyika pale tofauti zinapojitokeza ni kwanza kuzitambua na kuzielewa, pili kukubali kuwa si matatizo bali ni tofauti za kimaumbile, na tatu kutafuta namna ya kuchukuliana kwa hekima.
Kila mmoja anapaswa kuwa na nia ya dhati ya kumsaidia mwenzake kukabiliana na tofauti hizo, badala ya kumlaumu au kumwona kama chanzo cha shida. Ni muhimu pia kutambua kwamba njia iliyowasaidia wapenzi fulani kukabiliana na tofauti zao huenda isiwafae wengine, kwa sababu uhusiano nao hutofautiana kulingana na wahusika wake.
Hali inabadilika kabisa tunapokutana na matatizo ya kweli katika uhusiano. Matatizo hayatakiwi kuvumiliwa au kuzoelewa kwa kisingizio cha kuchukuliana, bali yanahitaji kutatuliwa. Tatizo hubaki kuwa tatizo milele hadi pale suluhisho la kweli litakapopatikana.
Njia sahihi ni kwenda kwenye mzizi wa tatizo, kulijadili kwa uwazi na kwa pamoja kutafuta ufumbuzi wa kudumu. Kujaribu kuyazoea matatizo ni kujidanganya na ni njia ya uhakika ya kujikusanyia majeraha ya moyo na kihisia.
Vivyo hivyo, kujaribu kuzitafutia suluhisho tofauti za kijinsia ni kupoteza nguvu na kuongeza msongo wa mawazo, hali ambayo mara nyingi husababisha uhusiano kuvunjika.
Katika uhusiano, yapo matatizo yanayojirudia kwa wapenzi wengi. Miongoni mwao ni uchafu au kutojali usafi, ubahili, hasira za haraka au za kupitiliza, uongo, upendeleo hasa kwa ndugu wa upande mmoja, wizi au udokozi, kutokuwa mwaminifu, pamoja na kunyimana au kutofurahia tendo la ndoa.
Haya ni matatizo halisi yanayohitaji kushughulikiwa kwa umakini na kwa uamuzi wa pamoja.Kwa upande wa tofauti, mifano yake ipo wazi katika maisha ya kila siku. Wanawake wengi hupenda kufanya manunuzi, hata yale yasiyo rasmi, na hupata furaha kwa kutembelea maduka au masoko ili kuangalia bidhaa na bei zake hata bila mpango wa kununua. Kwa wanaume, jambo hili huwa gumu kuelewa, hasa pale wanapojua hawana fedha au hawana mpango wa kununua chochote.
Wanaume, kwa asili, hupenda kupanga mambo kabla ya kuyafanya, wakihitaji mpango ulio wazi na wenye mwelekeo maalumu. Wanawake, kwa upande mwingine, mara nyingi huonekana kuwa watumiaji wazuri wa pesa bila kufungamana sana na bajeti au malengo yaliyowekwa, jambo linalosababisha migongano ya mara kwa mara katika masuala ya fedha.
Hali hii imewafanya baadhi ya wanawake kuwaona wanaume kama wabahili, huku wanaume wakilalamikia matumizi mabaya ya pesa.
Tofauti nyingine iliyo wazi ni katika mawasiliano. Wanawake kwa ujumla ni wawasilianaji wazuri zaidi kuliko wanaume. Wanapenda kuzungumza, kuelezea hisia zao na kushirikiana kwa kina.
Wanaume, kwa upande wao, huona ugumu katika kuzungumza kwa muda mrefu au kuelezea hisia zao waziwazi. Tofauti hii mara nyingi huwafanya wanawake wajisikie kama hawapendwi au hawathaminiwi, ilhali kwa mwanaume hali hiyo ni sehemu ya maumbile yake.
Kwa ujumla, tofauti za kijinsia ni nyingi na huendelea kujidhihirisha kadiri uhusiano unavyozidi kukua. Ukweli unaopaswa kukubalika ni kwamba ni vigumu sana kwa wapenzi wawili kufanana, lakini inawezekana kabisa kuendana.
Kadiri muda wa kuwa pamoja unavyoongezeka, na kila mmoja anapokuwa tayari kujifunza, kuvumilia na kuelewa, uhusiano unaweza kuwa na furaha na uthabiti licha ya tofauti zilizopo. Katika uhusiano, kuendana ni muhimu kuliko kufanana.
