Unajengaje ngome ya kihisia na usalama kwa mwenza

Katika ulimwengu wa sasa uliogubikwa na pilkapilka nyingi, ambapo muda umekuwa bidhaa adimu, uhusiano wa kimapenzi unajipata katika mtihani mzito.

Watu wengi wanaishi chini ya paa moja lakini wapo mbali kihisia; wanashirikiana majukumu ya kifedha na malezi, lakini mioyo yao haigusani.

Kujenga ukaribu wa kihisia na hali ya usalama si jambo linalotokea kwa bahati mbaya, bali ni mchakato wa makusudi unaohitaji maarifa, subira, na mbinu za kisayansi na kisaikolojia.

Usalama huu tunaozungumzia si wa kumlinda mwenza na majambazi, bali ni ule usalama wa moyoni, hali ambapo mwenza wako anajihisi kuwa anaweza kuwa yeye halisi bila kuhukumiwa, na kwamba hitaji lake la kupendwa litatimizwa kila anapohitaji.

Mwanasaikolojia mashuhuri Dk Sue Johnson, ambaye ni mwasisi wa tiba ya uhusiano inayozingatia hisia, anasisitiza kuwa binadamu ana hitaji la kiasili la kushikamana na mwingine.

Katika kitabu chake maarufu: Hold Me Tight, anaeleza kuwa migogoro mingi katika ndoa si matokeo ya kutoelewana kwa kawaida, bali ni kilio cha kutaka usalama wa kihisia.

Anafafanua kuwa pale mwenza anapohisi kutengwa, ubongo wake huingia katika hali ya taharuki. Katika kitabu hicho, anatoa kauli nzito anaposema: “Uhusiano wa kina ndio usalama pekee tulionao katika ulimwengu huu.”

Kwa mantiki hiyo, mbinu ya kwanza ya kujenga ukaribu ni kuwa “mwenye kupatikana.”

Hii ina maana kuwa wakati mwenza wako anapohitaji usikivu wako, unapaswa kuwepo si kimwili tu, bali pia kiroho na kihisia, ukimhakikishia kuwa yeye ni kipaumbele chako cha kwanza.

Hata hivyo, kuwepo pekee hakutoshi ikiwa hakuna uelewa wa jinsi mwenza wako anavyopokea upendo.

Hapa ndipo tunapokutana na mawazo ya Dkt Gary Chapman, mwandishi wa kitabu kilichouza mamilioni ya nakala, The 5 Love Languages. Chapman anajenga hoja kuwa kila mwanadamu ana “lugha ya mapenzi” ambayo akizungumziwa kwayo, anajihisi salama na kupendwa zaidi.

Chapman anasisitiza kuwa matatizo huanza pale wenza wanapozungumza lugha tofauti; mmoja anaweza kuwa anatoa zawadi (lugha yake), wakati mwenza anahitaji muda wa ubora (lugha ya mwenzake).

Katika kitabu chake, Chapman anaandika: “Upendo ni uamuzi unaofanya kila siku.” Hii inaashiria kuwa kujenga ukaribu wa kihisia ni juhudi za kila siku za kujifunza lugha ya mwenza wako na kuamua kuizungumza hata kama si ya asili kwako.

Unapojifunza kumpenda mwenza wako kwa namna anavyoelewa yeye iwe ni kwa maneno ya kutia moyo, matendo ya huduma, au kugusana, unakuwa umejenga ukuta imara wa usalama ambao ni vigumu kubomolewa na dhoruba za nje.

Mawasiliano na uvumilivu wa upungufu

Ukaribu wa kihisia unategemea sana jinsi wenza wanavyowasiliana wakati wa tofauti zao. Dk John Gottman, mtafiti ambaye amechunguza maelfu ya wanandoa kwa miongo kadhaa, anabainisha kuwa usalama wa kihisia hutoweka pale “farasi wanne wa maangamizi” wanapoingia ndani ya nyumba, akimaanisha ukosoaji, dharau, kujihami, na ukimya wa kususia.

 Katika kitabu chake, The Seven Principles for Making Marriage Work, anaeleza kuwa wenza walio karibu kihisia si wale wasiogombana, bali ni wale wanaojua jinsi ya “kukarabati” uhusiano baada ya kutofautiana. Dk Gottman anasisitiza umuhimu wa kujuana kwa ndani, kile anachokiita “Ramani ya Mapenzi” ambapo mwenza mmoja anajua ndoto, hofu, na matamanio ya mwenzake.

Anatoa ushauri muhimu akisema: “Ndoa yenye mafanikio haihusu kumpata mtu aliyekamilika, bali ni kujifunza kumpenda huyo mtu asiyekamilika uliyempata.”

Kwa kuukubali udhaifu wa mwenza wako na kuuheshimu, unamtengenezea mazingira salama ambapo hahitaji kujificha au kuvaa kificha uso.

Ukaribu wa kihisia unastawi pale mwenza anapojua kuwa hata akifanya makosa, hatadharauliwa wala kudhalilishwa.

Badala yake, mawasiliano ya upole na yenye staha yanakuwa daraja la kuunganisha mioyo iliyopishana.

Hii inahusisha pia sanaa ya kusikiliza kwa madhumuni ya kuelewa, si kusikiliza kwa kujibu au kushinda hoja, jambo ambalo mara nyingi huzua kuta badala ya madaraja.

Aidha, ukaribu huu unapaswa kuendana na hali ya kuaminika. Usalama wa kihisia unajengwa juu ya msingi wa uaminifu mdogo mdogo wa kila siku kama kutimiza ahadi, kuwa mkweli katika mambo madogo, na kuwa mlinzi wa siri za mwenza wako.

Unapokuwa mtu ambaye mwenza wako anaweza kumtegemea bila shaka, unakuwa umewekeza katika akaunti ya kihisia ambayo itawasaidia wakati wa mizozo mikubwa.

Ni lazima kutambua kuwa usalama si hali tuli, bali ni bustani inayohitaji palizi ya kila mara. Wenza wanapaswa kuwa na tabia ya “kuitikia miito”

Kwa mfano, mwenza wako anapokuonyesha kitu kwenye simu au kutoa maoni juu ya hali ya hewa, huo ni “mwito” wa kutaka ukaribu; kuitikia kwa hamu hujenga ukaribu, lakini kupuuza hubomoa usalama wa kihisia kidogo kidogo.

Ujasiri wa kuwa wazi na nguvu ya udhaifu katika uhusiano

Pengine sehemu ngumu zaidi lakini yenye tija katika kujenga ukaribu wa kihisia ni ujasiri wa kuonyesha udhaifu.

Brené Brown, mtafiti na mwandishi wa kitabu: Daring Greatly, amefanya kazi kubwa kueleza jinsi uoga wa kuonekana dhaifu unavyozuia watu kuwa karibu kihisia.

Watu wengi huvaa silaha za kujihami ili wasiumizwe, lakini silaha hizo hizo ndizo zinazozuia upendo na ukaribu kuingia.

Ili mwenza wako ajihisi salama kwako, ni lazima na wewe uwe tayari kuwa wazi kuhusu hofu zako, mashaka yako, na hata aibu zako. Brown anasema kuwa udhaifu si udhaifu wa tabia, bali ni kipimo cha juu kabisa cha ujasiri.

Katika maandiko yake, Brown anasema: “Udhaifu (kuwa wazi) ndipo mahali ambapo upendo, hali ya kuwa sehemu ya kitu, furaha, na ujasiri huzaliwa.” Unapomruhusu mwenza wako kuona sehemu zako ambazo hupendi kuzionyesha kwa ulimwengu, unamwalika katika chumba cha ndani kabisa cha moyo wako.

Kitendo hiki cha imani kinamfanya mwenza wako ajihisi kuwa naye anaweza kuweka chini silaha zake na kupumzika.

Hapo ndipo usalama wa kweli wa kihisia unapoishi yaani pale ambapo wote wawili mnajua kuwa mnaweza kuonekana mlivyo na bado mkapendwa kwa dhati.

Muhimu kukumbuka ujenzi wa ukaribu wa kihisia na usalama kwa mwenza ni safari ndefu inayohitaji mchanganyiko wa mambo mengi.

Uhusiano imara si ule usio na matatizo, bali ni ule ambapo wenza wameamua kuwa “bandari salama” kwa kila mmoja. Katika dunia yenye dhoruba nyingi, nyumba inapaswa kuwa mahali ambapo moyo unapata utulivu, na usalama huo unaanza na wewe kuamua leo kuwa mlinzi wa hisia za mwenza wako, ukimpa kipaumbele, ukimuelewa, na kumpenda katika uhalisia wake wote.

Makala haya kwa hisani ya vyanzo mbalimbali vya kimtandao.