Utamu wa Azam vs Yanga upo hapa

WALE ‘Wazee wa Mikeka’, ni wazi wikiendi hii watakuwa na kazi katika kusuka mkeka wa mechi ya Dar es Salaam Derby inayozikutanisha Azam FC na vinara wa Ligi Kuu, Yanga.

Hii ni mechi ngumu uwanjani kwa wachezaji wa timu zote, lakini hata kwa ‘Wazee wa Mikeka’ wana kibarua cha kusuka mikeka yao ili itiki, kwani wakibeti kizembe tu inaweza kula kwao kutokana na ukweli timu hizo hadi sasa ndizo hazijapoteza mechi katika msimu huu. Hili ni pambano la 35 kwa timu hizo tangu mwaka 2008, lakini likiwa ni la kwanza kwao kwa msimu huu, huku kumbukumbu zikionyesha msimu uliopita kila timu ilishinda mechi moja.

Hii ni Dabi iliyobebwa zaidi na namba, lakini kukiwa na rekodi tamu za kusisimua za misimu 17 tangu timu hizo zilipoanza kukutana katika Ligi Kuu Bara. Msimu uliopita timu hizo hazikuchekana, kwani kila moja ilishinda mechi ya ugenini, Azam ikianza na ushindi wa bao 1-0 kisha Yanga kujibu mapigo kwa ushindi wa mabao 2-1 uliochangia kuiongezea pointi zilizoipa ubingwa wa 31 na wa nne mfululizo. Mechi hizo zote zilichezwa Uwanja wa Azam Complex, Dar.

Timu hizo zinakutana kuanzia saa 2:30 usiku huku kila moja ikiwa na kocha mpya, Azam ikiwa na Florent Ibenge wakati Yanga ina Pedro Goncalves, lakini vikosi vikiundwa na mashine za maana zilizozifanya timu hizo kuwa pekee ambazo hazijaonja vopigo katika mechi za Ligi ya msimu huu. Ibenge na Pedro wanakutana kwa mara ya pili wakiwa na timu hizo baada ya vita yao katika fainali ya Kombe la Mapinduzi 2026 kumalizika kwa Yanga kushinda penalti 5-4.

Mechi hii ukiacha msako wa pointi tatu, pambano hili linatarajiwa kubebwa zaidi na maeneo mawili ya timu hizo, idara ya kiungo na lile la ushambuliaji ambalo zimeibeba katika mechi zilizopita za Ligi Kuu msimu huu.

Yanga inajivunia majembe kama Mohammed Damaro, Duke Abuya, Mudathir Yahya anayeijua nje ndani Azam FC, mbali ya Maxi Nzengeli na ingizo jipya, Buba Jammeh, huku eneo la ushambuliaji likiwa na Allan Okello, Laurindi Depu, Prince Dube na Emmanuel Mwanengo.

Licha ya kwamba Yanga itakosa mashine kadhaa kama mshambuliaji Clement Mzize na beki wa kati, Dickson Job walio majeruhi, lakini bado waliopo wana nafasi ya kuibeba timu katika mechi hiyo ambayo watakuwa wageni wa Wanalambalamba.

Kwa upande wa Azam, ina vifaa vya maana katika eneo la kiungo akiwamo Feisal Salum ‘Fei Toto’ aliyerejea kutoka kutumikia adhabu ya kadi nyekundu tangu mechi iliyopita ya Ligi Kuu dhidi ya Dodoma Jiji, James Akaminko, mkongwe Himid Mao, Yahya Zayd, Adolf Mtasingwa na Sadio Kanoute.

Eneo la ushambuliaji lina majembe ya maana kama Jephte Kitambala, Jean Jacques Ngita, Idd Seleman ‘Nado’, Zidane Sereri na Mzee Hassan ‘Aziz KI’ ambao wakiliamsha kisawasawa wanaweza kuipa Yanga wakati mgumu chini ya kipa Djigui Diarra.

Ukiacha rekodi zilizopo kwa sasa kwa timu hizo katika Ligi Kuu Bara msimu huu ya kutopoteza mechi yoyote, lakini kuna zilizowahi kuwekwa katika mapambano ya awali ya Dar Derby.

Kama umesahau ni kwamba Azam ndio iliyokuwa timu ya kwanza msimu uliopita kuitibulia Yanga katika Ligi Kuu kwa kuifunga baada ya kucheza mechi nane mfululizo ikiwa chini ya Kocha Miguel Gamondi ikishinda zote. Bao la Gibril Sillah lilitosha kutia dosari ubabe wa Yanga kabla ya Tabora United ambayo sasa ni TRA United kutonesha tena donda hilo Novemba 7, 2024 na kuwa vipigo vya mwisho kwa wababe hao katika Ligi Kuu tangu wakati huo hadi sasa.

Kwani baada ya Azam kuichapa na Tabora United (sasa TRA United) kutonesha mshono, Yanga haijapoteza tena mechi yoyote katika Ligi Kuu ikicheza jumla ya mapambano 33. Hata hivyo, ni kwamba katika mechi 34 zilizopita baina ya timu hizo, kuanzia msimu wa 2008-2009 Azam ilipopanda daraja hadi za msimu uliopita wa 2024-2025, Yanga imeonekana kuwa kinara kwa kushinda mara nyingi zaidi ya Azam.

Timu hiyo imeshinda mechi 14 wakati Azam ikishinda 11 tu, huku mapambano tisa yakiisha kwa sare za aina tofauti na anga ikifunga jumla ya mabao 44 dhidi ya 41 ya Azam kuonyesha timu hizi hazichekani pale zinapokutana, licha ya kwamba Yanga imevuna pointi 51 dhidi ya 42 za Azam.

Mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Mkenya Boniface Ambani ndiye wa kwanza aliyefunga katika pambano la Dar es Salaam Derby akifanya hivyo Oktoba 15, 2008 wakati Yanga ikishinda kwa mabao 3-1.

Ambani alifunga bao dakika ya 11 kisha kuongeza la pili dakika nne baadae kabla ya John Bocco kuifungia Azam bao la kufutia machozi dakika ya 30 na Castrol Mumbala kufunga la tatu la washindi dakika ya 88.

Mbali na kuwa mfungaji wa kwanza wa pambano hili la Dar Derby, lakini alikuwa ni mchezaji wa kwanza kufunga mabao mawili katika mechi mbili mfululizo za wababe hao, kwani katika mechi ya marudiano iliyopigwa Aprili 8, 2009, alifanya hivyo katika kipigo cha mabao 3-2 ilichopewa Yanga.

Ambani aliitanguliza Yanga kama ilivyokuwa katika mechi ya mkondo wa kwanza kwa mabao ya dakika ya 27 na 43 kabla ya Yahya Tumbo kujibu mapigo kwa mabao ya dakika 54 na 65 na Shaaban Kisiga ‘Marlon’ kumalizia bao la ushindi la dakika ya 60.

Ukiacha Mkenya Ambani kuweka rekodi ya kuwa mchezaji aliyefunga bao la kwanza la Dabi hiyo na kufunga mabao mawili mechi mbili mfululizo, lakini kiboko yo ni nahodha wa zamani wa Azam, John Bocco ‘Adebayor’ aliyejua kuitungua Yanga atakavyo.

Mwamba huyo ambaye kwa sasa ni kocha wa timu ya vijana ya Simba, amestaafu akiwa ameacha rekodi ya aina yake ya kuitungua Yanga jumla ya mabao 10 akiwa kinara wa mechi za Dar Derby akitumia misimu tisa akiwa Chamazi kabla ya 2017-2018 kuhamia Msimbazi.

Bocco alianza kuifunga Yanga katika mechi ya kwanza baina ya timu hizo msimu wa 2008-2009, Azam ilipolala mabao 3-1 na bao lake la mwisho dhidi ya Wanajangwani alilitupia Machi 05, 2016 akiiokoa timu hiyo na kipigo kwa kulazimisha sare ya mabao 2-2.

Katika mechi hiyo, beki Juma Abdul wa Yanga aliitanguliza Azam kwa kujifunga dakika ya 11 kabla ya Amissi Tambwe kuchomoa na Donald Ngoma kuongeza lingine kabla ya mapumziko, ndipo Bocco alifunga bao la kusawazisha dakika ya 70, likiwa bao la mwisho la dabi hiyo ya Dar es Salaam.

Nyota huyo aliyekuwa na kismati pia cha kuitungua Simba kabla ya kuhamia huko, aliwaacha wenzake mbali katika kutupia kwenye Dar Derby, kwani wachezaji waliomfuata ambao ni; Boniface Ambani (Yanga), Stephane Aziz KI (Yanga) na Didier Kavumbagu aliyezitumikia kwa wakati tofauti timu hizo kila mmoja amefunga mabao manne tu.

Kina Ambani wanafutiwa kwa karibu na Fiston Mayele na Hamis Kiiza (wote Yanga), Gibril Sillah (Azam) pamoja na Feisal Salum na Prince Dube waliotupia wakiwa na timu hizo kwa misimu tofauti kila mmoja akiwa na mabao matatu.

Ni Dube na Feisal sambamba na Mudathir Yahya, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Farid Mussa waliowahi kufunga mechi zilizopita ndio wachezaji pekee walioopo sasa walizozitumikia timu hizo mbili kwa vipindi tofauti.

Beki na nahodha wa zamani wa Yanga, Juma Abdul ndiye aliyekuwa mchezaji wa kwanza kujiweka mwenyewe wavuni katika Dar Derby akifanya hivyo Machi 5, 2016, wakati timu hizo zikitoka sare ya 2-2 kabla Abdallah Kheri wa Azam naye kujiweka katika ushindi wa mabao 3-1 iliyopata timu hiyo ya Chamazi katika mechi iliyopigwa, Mei 28, 2018.

Beki mwingine kujiweka alikuwa ni Ally Mtoni ‘Sonso’ (sasa marehemu) wakati Yanga ikilala bao 1-0 katika mechi iliyopigwa Januari 18, 2020, akiwa ndiye nyota wa mwisho kufanya hivyo, huku mchezaji wa mwisho kufunga katika mechi za Dar Derby ni nahodha wa Azam, Lusajo Mwaikenda.

Lusajo alifunga wakati Azam ikizamishwa mabao 2-1 katika mechi ya marudiano ya msimu uliopita iliyopigwa Aprili 10, 2025 ambapo Yanga ilitangulia kwa mabao ya Pacome Zouzoua dakika ya 11 na Prince Dube dakika ya 33 kabla ya beki huyo kutupia la kufutia machozi dakika ya 81 ya pambano hilo.