Arusha. Watu wanne wamefariki dunia wilayani Monduli mkoani Arusha kufuatia mvua kubwa zilizosababisha mafuriko katika baadhi ya maeneo.
Mafuriko hayo pia yamesababisha uharibifu wa miundombinu na mali za wanafunzi katika Shule ya Msingi Engaruka Juu, hali iliyosababisha shule hiyo kufungwa kwa muda.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili Machi 15, 2026, Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Gloriana Kimath amesema wanaendelea kutoa elimu ya tahadhari kwa wananchi hususan wanaoishi maeneo hatarishi kutakiwa kuhama.
Mkuu huyo wa wilaya ametoa tahadhari kwa wananchi kuwa makini wanapokuta maji mengi maeneo yenye makorongo na mito, akisema baadhi ya vifo hivyo vimetokana na watu kuvuka maeneo yenye maji wakidhani wanaweza kupita kama ilivyokuwa miaka iliyopita.
“Wananchi wanapokutana na maji kwenye maeneo ya makorongo wasivuke, kwa sababu kuna baadhi ya maeneo vifo vimesababishwa na watu kutojali wakawa wanavuka kwa uzoefu kwamba miaka yote wanapita hata kama mvua zinanyesha na maji yanatembea, taarifa niliyonayo hadi sasa watu wanne wameshafariki dunia,” amesema mkuu huyo wa wilaya.
Aidha, amesema mvua hizo zimesababisha madhara katika Shule ya Msingi Engaruka Juu ambako baadhi ya miundombinu ya shule na mali za wanafunzi zimeharibika.
Amesema kutokana na hali hiyo, shule hiyo imefungwa kuanzia Machi 10 hadi Machi 18 mwaka huu ambapo itafunguliwa kwa madarasa ya mitihani (darasa la nne na la saba).
“Wanafunzi wameharibiwa mali zao vikiwamo vitanda, matranka, magodoro na choo kimoja cha matundu nane kiliingia tope. Pia baadhi ya vitabu vimeharibika baada ya chumba cha kuhifadhia vitabu kuingia tope,” amesema Limath.
Amesema kwa sasa kinachoendelea shuleni hapo ni kazi ya usafi pamoja na ukarabati wa milango, madirisha na vitanda na wanaendelea kupokea misaada kutoka kwa wadau mbalimbali kama madaftari na mashuka ili kusaidia wanafunzi walioathirika.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo, Shule ya Msingi Engaruka Juu ina wanafunzi zaidi ya 1,400 huku zaidi ya wanafunzi 200 wakiwa ni wa bweni.
Hata hivyo amesema huduma katika vituo vya afya zinaendelea kama kawaida licha ya baadhi kuzingirwa na maji kwa muda mfupi.
“Kwa maana ya kutofanya kazi kabisa hapana, isipokuwa kuna baadhi ya vituo vya afya vilizingirwa tu na maji kwa muda, lakini kwa sasa hakuna shida ikiwemo Mto wa Mbu, Engaruka na Selela,” amesema.
Kimath amewataka wananchi wa maeneo mbalimbali, hususan wakulima wa migomba katika eneo la Mto wa Mbu, kuepuka kutupa mabaki ya migomba kwenye mifereji ya maji kwa sababu husababisha kuziba na kuongeza hatari ya mafuriko.
