Watafiti wabaini aina sita za uyoga zinazopatikana Tanzania pekee

Morogoro. Wataalamu na watafiti wa uyoga pori, wamesema tafiti mbalimbali zilizofanywa zimebaini kuwepo kwa aina sita za uyoga zinazopatikana Tanzania pekee, hali inayoiweka nchi katika nafasi nzuri ya kukuza zao hilo katika soko la kimataifa.

Sambamba na hilo, wamesema wameanza mkakati wa kuongeza tafiti za kisayansi ili kuimarisha uzalishaji wa zao hilo kibiashara na kulipendekeza liingizwe katika orodha ya mazao ya kimkakati nchini.

Mkakati huo ulijadiliwa katika kikao kazi cha jukwaa la wadau wa uyoga kilichowakutanisha watafiti, wajasiriamali na wadau wa sekta hiyo kwa lengo la kupitia rasimu ya katiba ya jukwaa hilo pamoja na kujadili namna bora ya kuongeza thamani ya zao hilo.

Akizungumza katika kikao hicho, Profesa wa Sayansi ya Uyoga katika Idara ya Sayansi za Mimea ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Donatha Tibuhwa amesema tafiti mbalimbali zilizofanywa zimebaini kuwepo kwa aina sita za uyoga zinazopatikana Tanzania pekee.

Amesema tafiti hizo pia zimechangia kuanzishwa kwa kilimo cha uyoga nchini ambacho kimekua kwa kasi tangu kuanza kwake mwaka 1993.

“Utafiti umechangia kuanzishwa kwa kilimo cha uyoga kutoka wakulima sifuri mwaka 1993 hadi zaidi ya wakulima 5,000 kwa sasa na kuna aina saba za uyoga ambazo zikifanikiwa kufanyiwa domestication na kuonesha faida kubwa zitasaidia uchumi na kiafya,” amesema.

Hata hivyo, wadau wa zao hilo, wameeleza kuwepo kuna changamoto mbalimbali zinazokwamisha maendeleo ya uzalishaji wa uyoga, ikiwamo athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na shughuli za kibinadamu katika misitu ya Miombo ambako uyoga huo hupatikana.

Baadhi ya wajasiriamali wa zao hilo kutoka Mkoa wa Tabora, Catherine Changoma na Neema Maganga, wamesema licha ya kupata mafunzo ya uzalishaji na uhifadhi wa uyoga kupitia Asasi ya ADAP, bado wanakabiliwa na changamoto za mazingira zinazopunguza uzalishaji.

Amesema kuingizwa kwa mifugo katika misitu ya Miombo kunaharibu mazalia ya uyoga kutokana na kwato za mifugo kukanyaga maeneo ambayo uyoga huota.

“Uyoga pori hupatikana kwenye misitu ya Miombo, lakini wafugaji wanapoingiza mifugo kutafuta malisho, kwato zao huharibu kabisa mazalia ya uyoga na kufanya uzalishaji kupungua,” amesema Changoma.

Ameiomba Serikali na wadau wa sekta hiyo kusaidia kuwafungulia masoko makubwa zaidi ikiwamo ya kimataifa ili wajasiriamali wa zao hilo waweze kuongeza kipato chao.

“Licha ya kuwepo kwa soko la ndani, bado baadhi ya jamii nchini hazijatambua kikamilifu umuhimu wa uyoga katika lishe na afya ikilinganishwa na mataifa mengine,” amesema Changoma.

Ameongeza kwa kusema kuwa, kuna umuhimu na faida kwa kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu faida za uyoga, kuwa baadhi ya aina zake husaidia kuongeza lishe na hata kuchochea uzalishaji wa maziwa kwa mama baada ya kujifungua.

Kwa upande wake, Neema Maganga aliomba Serikali na mamlaka husika kuchukua hatua za kudhibiti mifugo kuingia katika maeneo ya misitu ili kulinda mazalia ya uyoga.

Amesema kupitia kikundi chao cha Tushikamane, wamefanikiwa kuongeza kipato na kuwasaidia watoto wao kupata elimu kupitia shughuli za uzalishaji na uuzaji wa uyoga.

“Zao hili limetusaidia kuongeza kipato cha familia na kuwapeleka watoto shule, hivyo tunahitaji mazingira bora zaidi ya kulikuza,” alisema Maganga.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Mazao ya Misitu (Tafori), Dk Revocatus Mushumbusi, amesema taasisi hiyo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inaendelea kuimarisha tafiti zitakazosaidia kuongeza uzalishaji na thamani ya uyoga nchini.

Amesema Tafori imekuwa ikishirikiana na taasisi mbalimbali za kitaaluma zikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela na Asasi ya Uhifadhi kwa Uendelevu wa Maeneo Yaliyohifadhiwa (ADAP).

“Lengo ni kufanya tafiti zitakazokuja na suluhisho la kuongeza uzalishaji, thamani na soko la uyoga ili liweze kuwa zao lenye mchango mkubwa katika uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla,”amesema Dk Mushumbusi.