Yalipo mabao dabi ya Azam vs Yanga

AZAM na Yanga zinakutana tena uwanjani Jumapili hii Machi 15, 2026 katika msako wa pointi tatu ndani ya Ligi Kuu Bara baada ya kupita kipindi cha takribani siku 61 tangu zilipotoana jasho kwenye fainali ya Kombe la Mapinduzi 2026.

Ndani ya siku 61 ambazo timu hizo tangu mara ya mwisho zikutane, kuna mambo mengi hapo kati yametokea, huku leo ikisubiriwa nani ataibuka mbabe. Pedro Goncalves na kikosi chake cha Yanga kitaendeleza umwamba, au Florent Ibenge na vijana wake wa Azam watakataa unyonge? Dakika tisini zitaamua.

Kuelekea mechi hii itakayoanza saa 2:30 usiku ikichezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, kuna nyota ambao wana takwimu nzuri zinazowapa nafasi kubwa ya kuamua mechi ambapo huenda wachezaji hao ndiyo watafunga au kutengeneza nafasi za kufunga.

Katika orodha ya mabao, Feisal Salum ‘Fei Toto’ (Azam), Prince Dube na Laurindo Dilson ‘Depu’ wote wanaocheza Yanga wana sita, wanaingia kwenye mechi hii kama vinara wa ufungaji. Chini yao kuna Iddy Selemani ‘Nado’ wa Azam mwenye matano, kisha Jean Jacques Ngita (Azam) na Mudathir Yahya (Yanga) kila mmoja anayo manne, huku Pacome Zouzoua wa Yanga anayetarajiwa kucheza mechi hii baada ya kupona majeraha yake ana mabao matatu.

Ishu ya kutengeneza mabao kwa maana ya asisti, Fei Toto anaongoza tena akiwa na tano, anafuatiwa na Duke Abuya wa Yanga mwenye nne, kisha nyota wawili wa Yanga, Maxi Nzengeli na Israel Mwenda wenye tatu kila mmoja. Wenye asisti mbili ni Lusajo Mwaikenda (Azam) na Pacome Zouzoua (Yanga).

Hata hivyo, ushindi unaosubiriwa leo unaweza kuwa zaidi ya ule tulioushuhudia kwenye fainali ya Kombe la Mapinduzi 2026 iliyochezwa kwa dakika 120 bila bao kupatikana, kisha Yanga ikashinda kwa penalti 5-4.

Wakati ule, Ibenge alikuwa na kikosi chenye mchanganyiko wa vijana na wakongwe, huku Yanga asilimia kubwa ikishusha jesho lake la kazi ambalo Pedro ameliambinia hadi sasa linampa matokeo mazuri.

Hata hivyo, mechi hii Ibenge anaweza kuingia tofauti sana na hapo awali alipopoteza mbele ya Pedro, huku uwepo wa kinara wa asisti, Feisal Salum mwenye tano na moto wa Laurindo Depu pale Yanga akiingia dirisha dogo na kufunga mabao sita, unatajwa kuleta mvuto zaidi.

Uzuri wa mechi hii, tunakwenda kushuhudia timu ambazo msimu huu katika Ligi Kuu Bara ndizo pekee hazijapoteza mechi hadi sasa, Yanga ikiwa kileleni na pointi 35, Azam inazo 27 ikikamata nafasi ya tatu, ikifuatiwa na Simba (27). JKT Tanzania ipo nafasi ya pili na pointi 28.

Ukiweka kando hilo la kutopoteza, Azam na Yanga zimetoka kushinda mechi za mwisho tena zote zikichezwa Uwanja wa Jamhuri, Dodoma. Ilianza Azam kuichapa Dodoma Jiji mabao 3-0, kisha Yanga ikaifunga Tanzania Prisons 1-0.

Matokeo hayo yamechochea zaidi Dabi hii ya Dar es Salaam tunayokwenda kuishuhudia baada ya kipindi cha takribani wiki mbili zimepita tangu kuiona Dabi ya Kariakoo iliyomalizika kwa Yanga na Simba kutofungana ikichezwa Machi Mosi, 2026 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Makocha wa timu zote mbili wana mbinu zinazotifautiana kiuchezaji ambapo Ibenge anapendelea mfumo wa 4-2-3-1, hapo kati kuna viungo wawili wakabaji na kiungo mmoja mbunifu mbele yao. Kushoto na kulia mawinga wanaomlisha mshambuliaji mmoja mbele. Kule nyuma mabeki ni wanne.

Mfumo huu unamruhusu kudhibiti eneo la kati huku akitengeneza nafasi za masha mbulizi kupitia pembeni.

Kwa upande wa Yanga, kocha Pedro mfumo wake ni 4-3-3, wanapokuwa na mpira mara nyingi hubadilika na kuunda umbo la 2-4-1-3 au wakati mwingine 2-4-4.

Katika mfumo huo mama, walinzi wanakuwa wanne, kisha viungo wenye asili ya kukaba watatu akiwatumia Mudathir Yahya, Duke Abuya na Mohamed Damaro. Kule mbele kuna nyota watatu wa kushambulia. Allan Okello, Maxi Nzengeli na Prince Dube kama ambavyo alifanya mechi iliyopita dhidi ya Tanzania Prisons. Pia amewahi kujaribu washambuliaji wawili mbele, Dube na Laurindo Depu.

Akizungumzia mechi hiyo, Kocha wa Azam, Florent Ibenge alisema: “Kesho tunakwenda kucheza mpira, kuchukua pointi kama kawaida, hivyo tutacheza mchezo kamili na kuonyesha jinsi tunavyoweza kuwa bora.

Kwa upande wa Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves, alisema: “Tunakwenda kukutana na timu ngumu zaidi kwenye ligi, ni timu imara sana hasa ukizingatia ufanisi wao kwenye mashindano ya kimataifa, tulicheza nao kwenye fainali ya Kombe la Mapinduzi, nadhani wakati huu watakuja wamejipanga vyema zaidi.

“Tunakwenda kucheza na timu ngumu kwenye mazingira ambayo hatujayazoea kwa muda tokea nimekuwa kocha wa timu hii, ni mara ya kwanza nakwenda Uwanja wa Mkapa.

“Kucheza Uwanja wa Mkapa ni fursa nzuri sana kwetu, ni uwanja mzuri hivyo tumejiandaa vyema ili kupata matokeo mazuri.

“Kuna changamoto ndogo ndogo hasa ukizingatia ugumu wa mchezo uliopita na safari nzima basi utagundua kuwa wachezaji watakumbana na uchovu, tumepata muda wa kufanya maandalizi ya kuweka miili sawa tayari kwa mapambano.

“Cha ngamoto kubwa ambayo wachezaji wangu wanakumbana nayo ni kucheza katika mazingira tofauti tofauti ya viwanja, unacheza kwenye viwanja vibaya wakati mwingine viwanja vizuri. Ni lazima uwe na wachezaji wenye uelewa mkubwa kwa kimbinu ili kukabiliana na vikwazo vya viwanja.”