Arusha. Yasini Ramadhan (38), dereva bodaboda na mkazi wa Sakina jijini Arusha, anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kuwabaka watoto wake wawili wa kike, mmoja mwenye umri wa miaka sita na mwingine miezi saba.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo leo Jumatatu, Machi 16, 2026 na kusema upelelezi wa kina dhidi ya tuhuma hizo unaendelea.
“Upelelezi na mahojiano yanaendelea, na kama akibainika kutekeleza vitendo hivyo, sheria itachukua mkondo wake,” amesema.
Kamanda Masejo ametumia nafasi hiyo kuwataka wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kutoa taarifa za matukio ya kihalifu katika mkoa huo, ili kudhibiti na kuhakikisha usalama.
Awali, wakizungumza katika eneo la tukio, mke wa mtuhumiwa, Zanura Rashid, amedai mumewe alianza kufanya ukatili huo mwaka 2025 kwa mtoto wao mkubwa, akiwa na umri wa miaka mitano.
“Huwa tunalala pamoja na watoto kitanda kimoja, wao katikati na sisi pembeni, lakini siku moja mtoto huyo akaniambia baba amemfanyia kitendo hicho nikiwa nimelala.
“Nilimuangalia mtoto, kweli akaonekana ameingiliwa na amechubuka. Nilimkanda mtoto kwa maji ya vuguvugu na kumpumzisha shule siku mbili, akapona,” ameeleza.
Amedai baada ya siku nne, mtoto huyo alilalamika kufanyiwa tena kitendo hicho na baba yake.
“Huyu baba ni mkorofi na mlevi sana. Awali sikutaka ugomvi kutokana na mimba kubwa niliyokuwa nayo, lakini baada ya kuona mambo yanazidi, niliamua kumuuliza, naye alikataa katakata,” amesema mama huyo.
Amesema aliamua kuvumilia na kumhamisha mtoto upande mwingine hadi alipojifungua salama.
“Kilichonishinda kuvumilia ni leo kurudia na kunituma buchani kununua nyama, huku nyuma akafunga mlango na kumuingilia mtoto mdogo, akaondoka.
“Niliporudi tu, dada mkubwa akasema baba amemuingilia mdogo wake wa miezi saba, huku yeye akiamrishwa kufunga macho,” amesema.
Ameeleza kuwa baada ya kupewa taarifa hizo na kumkagua mtoto aliyekuwa alia muda wote, aliona ishara za kuingiliwa, ndipo akapiga kelele, majirani walikwenda kuona kilichotokea.
Mmoja wa majirani, Pendo Kwayu, amesema baba huyo amekuwa na tuhuma za kumwingilia mtoto wake mkubwa tangu mwaka jana, lakini walishindwa kupata uthibitisho wa awali.
“Leo tumesikia kelele kutoka kwa mama mzazi wa watoto, na baada ya kuja eneo la tukio, tukaona hali hiyo na kuanza kumsaka mtuhumiwa kabla hatujamkamata kwenye kijiwe chake cha bodaboda,” amesema.
Amesema baada ya kipigo kikali, mtuhumiwa alikiri kutekeleza tukio hilo kwa mtoto mkubwa pekee.
“Amekiri kumbaka mtoto mkubwa wa kike mara kadhaa, akisingizia ni pombe zilizomsababisha, lakini anakataa kumuingilia huyu mdogo, wakati tunaona wazi kuwa njia zake zimetanuka na kuna michubuko ya sehemu za siri,” amesema.
Jirani mwingine, Japhari Jona, ameliomba Jeshi la Polisi kumchukulia hatua kali za kisheria, akibainika kufanya tukio hilo, ili iwe fundisho kwa jamii nzima.
Katika ukurasa wake wa Instagram, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima, amewapongeza wakazi wa Arusha kwa kufichua tukio hilo na kuwataka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kuhakikisha mtuhumiwa anachukuliwa hatua za kisheria.
“Nawapongeza Arusha, kweli mko juu na somo linaeleweka. Wameanza kukataa ukatili, kitendo alichofanya baba huyo kilaaniwe, na sheria ifuate mkondo wake haraka,” amesema Dk Gwajima, akiwatag Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Maendeleo ya Jamii.
