BODI MPYA YA NCT YATAKIWA KUSIMAMIA UBORA NA UKARIMU KWA WATEJA

……………

Na. Sixmund Begashe, DSM

Bodi mpya ya Ushauri ya Wizara ya Wakala wa Chuo cha Utalii Tanzania , imeelekezwa kufanya tafiti na kuboresha mitaala ya Chuo hicho ili kiendelee kuzalisha wataalam wenye sifa na ubora zaidi hususan katika eneo la huduma kwa wateja na ukarimu.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) Jijini Dar es Salaam alipokuwa akizindua bodi hiyo yenye wajumbe 7. 

Dkt. Kijaji amesema kuwa, kazi kubwa imefanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutangaza vivutio vya utalii, hali inayopelekea watalii wengi kumiminika nchini, hivyo ni vyema chuo hicho kikaliangalia ipasavyo eneo la ubora wa huduma kwa wateja na ukarimu.

” Uwepo wa wataalam hao kutaendelea kushawishi watalii kurejea nchini kwa ajili ya kutembelea vivutio vyetu na hivyo kutuwezesha kufikia lengo tulilowekewa la watalii milioni 8 ifikapo Mwaka 2030″. Alisema Dkt. Kijaji

Aidha Dkt. Kijaji ameupongeza  uongozi wa Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) pamoja na Watumishi wote kwa kazi nzuri wa nayoendelea kuifanya na kuwataka waongoza juhudi hususani katika kutafiti zaidi kuhusu changamoto inayoikabili eneo la ukarimu. 

“Kwa upande wa Bodi hakikisheni mnaendelea kusimamia Menejimenti ya Chuo kikamilifu ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi ikiwa ni pamoja na kuangalia maslahi ya watumishi”.  Alisisitiza Dkt. Kijaji

Naye Mwenyekiti wa Bodi hiyo Dkt. Sharifa Omar Salim ameushukuru uongozi wa Wizara  kwa imani kubwa waliyoipa bodi hiyo na kuwa watahakikisha wanatekeleza maelekezo yote waliyopata ili kutimiza malengo yaliyo kusudiwa kwa maslahi mapana ya utalii endelevu nchini. 

Hafla ya uzinduzi wa Bodi hiyo imeudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Bw. Nkoba Mabula, baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya Wizara, viongozi na wataalam wa NCT.