Chadema yamtilia shaka Mwakilishi UN

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeonesha wasiwasi wa kuwepo kwa mgongano wa masilahi dhidi ya Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa (UN), Parfait Onanga-Anyanga, aliyetumwa kuzungumza na makundi mbalimbali nchini kuhusu matukio ya Oktoba 29.

Onanga-Anyanga, amefanya ziara hiyo Machi 8 hadi 12, mwaka huu na kuzungumza na wadau mbalimbali, wakiwamo viongozi wa Chadema, ACT Wazalendo, Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais Samia Suluhu Hassan, Spika wa Bunge, Mussa Zungu na Jaji Mkuu, George Masaju.

Katika wasiwasi wake huo, Chadema inasema kuna shaka ya kuwepo mgongano wa masilahi katika mchakato unaofanywa na Onanga-Anyanga, kwa kuwa ana historia ya uhusiano wa kikazi na Katibu Mkuu wa sasa wa CCM, Dk Asha-Rose Migiro.

Kihistoria, wawili hao waliwahi kufanya kazi katika ofisi ya Umoja wa Mataifa (UN) kwa miaka mitano yaani 2007 hadi 2012.

Wakati huo, Dk Migiro alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, huku Onanga‑Anyanga, akiwa Mkurugenzi wa Ofisi ya Naibu Katibu Mkuu wa UN, akisimamia masuala ya siasa na utawala.

Kutokana na hilo, Chadema Machi 12, 2026 imewasilisha barua kwa Katibu Mkuu wa UN, António Guterres, kikionyesha wasiwasi huo, huku kikiomba uchunguzi huru dhidi ya matukio ya Oktoba 29.

Oktoba 29, mwaka jana, kulitokea maandamano yaliyozaa vurugu na kusababisha vifo vya watu, uharibifu wa mali za umma na za watu binafsi.

Katika barua hiyo, Chadema imeonesha wasiwasi kuhusu taswira ya kuwepo mgongano wa masilahi katika mchakato unaoongozwa na Onanga-Ayanga, kutokana na uhusiano wake wa awali wa kikazi na Katibu Mkuu wa CCM, Dk Asha-Rose Migiro.

Imesema ingawa haiamini kwamba kunaweza kuwa na ushawishi wa moja kwa moja, uhusiano wa wawili hao unaibua wasiwasi kuhusu imani ya umma katika mchakato huo.

Kutokana na mazingira hayo, Chadema imemwomba Guiteres, kuwezesha kuundwa kwa Tume Huru ya Uchunguzi ya Umoja wa Mataifa, itakayojumuisha wanasheria na wataalamu wa kimataifa wanaoheshimika.

Tume hiyo, chama hicho kimetaka ifanye uchunguzi ili kubaini ukweli kuhusu matukio ya vurugu za Oktoba na Novemba mwaka jana na mwenendo wa watu kupotea tangu 2015, kukosekana kwa mageuzi ya kikatiba na ya uchaguzi.

Katika barua hiyo, Chadema kimesema kwenye mazungumzo yake na Onanga-Anyanga, kimewasilisha maoni ya kuachiwa huru bila masharti kwa mwenyekiti wao, Tundu Lissu na kurejeshewa haki zake za msingi.

“Kuondolewa kwa vikwazo vyote vilivyowekwa dhidi ya Chadema ili chama kifanye shughuli zake kwa uhuru kwa mujibu wa sheria,” imeeleza barua hiyo.

Pia, kimeomba kuundwa kwa tume huru, isiyoegemea upande wowote na yenye hadhi ya kimataifa kuchunguza mauaji ya Oktoba hadi Novemba mwaka jana.

Ilichosema Chadema yenyewe

Alipotafutwa kuzungumzia hilo, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, Amani Golugwa amekiri chama chake kuwasilisha barua hiyo na kwamba imepokewa.

“Imepokewa kwa maana ofisi ya Katibu Mkuu wa UN ameipokea barua ambayo ina maudhui tuliyoyaandika,” amesema.

Katika ufafanuzi wake, amesema msingi wa barua ni kutaka uhakika na juhudi zozote zinazofanywa na jumuiya ya kimataifa, hazitakatishi makosa yaliyofanywa Oktoba 29, 2025.

“Wala hatuko kinyume na juhudi zinazofanywa, lakini tuko makini kuhakikisha juhudi zozote zinafanywa katika mazingira ya kuaminika na kuheshimika ili wanaopaswa kuwajibika wawajibike au wawajibishwe,” amesema.

Hadi wanaandika barua hiyo, amesema wasiwasi wao ni uhusiano wa kikazi aliokuwa nao Onanga-Anyanga na Dk Migiro, kwani wawili hao waliwahi kufanya kazi pamoja.

“Mwaka 2007 hadi 2012 Onanga-Anyanga alikuwa msaidizi wa Dk Migiro kabla hajawa Katibu Mkuu wa CCM, kwa sababu hiyo, uaminifu wake unakuwa na mgongano wa maslahi,” amesema.

Lakini, kwa kuwa barua imepokewa, amesema anaamini mifumo ya UN itaendelea kutimiza wajibu wake ili mambo mengine yaendelee.