Daraja Mkuyuni limekamilika na limeanza ‘kulipa’- Ulega

Mwanza. Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesema kukamilika kwa ujenzi wa Daraja la Mkuyuni mkoani Mwanza, tayari kumeanza kuonyesha matunda katika siku zake za awali.

Akizungumza na wananchi mara baada ya ukaguzi wa daraja hilo leo Jumatatu, Machi 16, 2026 Ulega amesema wakazi wa Mwanza ni mashahidi wa hali hiyo hasa kufuatia matukio ya karibuni ya mvua kubwa zilizonyesha ambapo kama kusingekuwa na daraja, maafa makubwa yangetokea.

“Kwa wastani mvua hapa hunyesha kwa wastani wa milimita 140. Hii ya wiki jana watu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa wanasema kiwango kilikuwa ni milimita 185. Hiki ni kiwango kikubwa ambacho hakijawahi kutokea katika miaka ya karibuni.

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega akizungumza wakati akikagua Daraja la Mkuyuni mkoani Mwanza.

“Kuna picha mjongeo zilirushwa kwenye mitandao kuonyesha daraja halijafaa. Hao ni watu wa nje ya Mkuyuni. Watu wa hapa wanajua nini ambacho hili daraja limewafanyia,” amesema Ulega.

Daraja hilo ambalo ujenzi wake ulianza Novemba 2024 na kugharimu Sh5 bilioni, ni sehemu ya miradi ya dharura 81 ambayo Rais Samia Suluhu Hassan aliagiza ijengwe kwa thamani ya zaidi ya Sh560 bilioni ili kuboresha miundombinu iliyoathiriwa na mvua na vimbunga miaka miwili iliyopita.

Katika mkutano huo, Ulega amesema ni muhimu kwa wananchi kuwa watetezi wa kwanza wa miradi ya Serikali kwa kuwajibu watu wanaopotosha ambao, kwao serikali haina jambo jema inalowafanyia wananchi.

Ulega alitembelea daraja hilo ikiwa ni sehemu ya maelekezo aliyopewa na Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba, kuhakikisha ujenzi wake unakamilika haraka ili kuondoa usumbufu kwa wananchi.

Mwonekano wa Daraja la Mkuyuni mkoani Mwanza.

Baada ya ukaguzi wa leo, Ulega amesema sasa atafikisha salamu kwa Dk Mwigulu kuwa kazi hiyo iliyofanywa na mkandarasi mzalendo wa kampuni ya JASCO sasa imekamilika rasmi – ikiwemo ufungwaji wa taa za barabarani.

Katika hatua nyingine, Ulega ametoa mchango wa Sh5 milioni kwa ajili ya kusaidia wafanyabiashara wadogo ambao biashara zao ziliathiriwa na mafuriko ya wiki iliyopita.

“Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan inajali utu. Nafahamu kuwa hatuwezi kurejesha kila kilichopotea lakini, tunachoweza kufanya ni kuonyesha utu kwa wenzetu waliokumbwa na kadhia hiyo,” amesema.

Akitoa taarifa kuhusu daraja hilo, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mwanza, Paschal Ambrose, amesema daraja hilo lina upana wa mita 15 na njia sita – nne za magari na mbili za watembea kwa miguu.

Amesema kukamilika kwa daraja hilo kutafungua zaidi njia ya usafiri wa barabara kati ya mikoa ya Mwanza na Shinyanga na kwamba, itakuwa na msaada mkubwa hasa katika nyakati za masika ambako eneo la Mkuyuni lilikuwa likifahamika kwa kutopitika.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi, alisema wananchi wa Nyamagana wanamshukuru Rais Samia kwa ujenzi wa daraja hilo kwani, litakuwa na msaada mkubwa kwao.

“Hili daraja kama lingekuwa halipo, huenda hadi leo eneo la Makuyuni lingekuwa halipitiki kwa sababu ya wingi wa maji hasa wakati wa mvua,” amesema Makilagi.