Familia yaiangukia Serikali kupotea kwa mtoto wao

Mbeya. Zikiwa zimepita siku 12 tangu kutoweka kwa mtoto Frank Aliko (10), familia yake imeiangukia Serikali ikiitaka kufanya uchunguzi wa kiintelenjia kufanikisha kupatikana kwake.

Frank (10), mwanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Ikulu iliyopo Kata ya Ilomba, Halmashauri ya Jiji la Mbeya, inadaiwa ametoweka nyumbani tangu Machi 4, 2026 baada ya kupelekwa shuleni na kaka yake, lakini hakurejea tena.

Imeelezwa ni siku 12 sasa familia imegubikwa na giza nene kuhusu aliko mtoto huyo kumsaka bila mafanikio.

Hata hivyo, jitihada za Mwananchi kumpata Kamanda wa Polis Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga ili kuzungumzia suala la kupotea kwa mtoto huyo, hazikuzaa matunda na alipopigiwa simu na kutumiwa ujumbe mfupi wa maandishi, hakujibu.

Akizungumza na Mwananchi Ieo Machi 16, 2026, baba mzazi wa mtoto huyo, Aliko Fwanda amesema kwa sasa familia iko njia panda haitambua hatima ya kupatikana kwake.

“Awali Machi 4, asubuhi, kuna utaratibu nimeweka nyumbani kwangu, kaka yake hubeba jukumu la kumpeleka shuleni kila siku na baadaye kuendelea na majukumu yake ya kiuchumi,” amesema.

Fwanda amesema siku ya tukio, tangu alipoenda shuleni hakurejea tena, ndipo walianza jitihada za kumsaka maeneo mbalimbali ikiwepo kwa ndugu bila mafanikio.

“Kimsingi akili yangu haipo sawa, kama familia tumezunguka kila maeneo hususani hospitalini, vyumba vya kuhifadhia maiti bila matumaini, jambo ambalo sasa hatuna namna ni vyema kuomba msaada kwa Serikali,” amesema.

Kuhusu kutoa taarifa Polisi

Fwanda amesema awali baada ya mtoto wake kutorejea nyumbani, alitoa taarifa Kituo cha Polisi Ilomba na kupewa barua yenye kumbukumbu namba ILO/RB /282/2026 huku akitakiwa kurejea ndani ya saa 48 endapo hajapatikana, jambo ambalo alilitekeleza.

“Kwa sasa tupo njia panda, hatuelewi twende wapi maana maeneo yote muhimu mtu akipotea tumefika iwe kwa baskeli, bodaboda na gari bila mafanikio,” amesema.

Aliko amesema awali mtoto huyo alikuwa akiishi upande wa mzazi mwenzake, baada ya kuona maendeleo ya masomo sio mazuri alimuomba ili kumsimamia aweze kufanya vizuri katika mtihani wake wa kuhitimu elimu ya msingi.

Akizungumza na Mwananchi, Mwalimu Mkuu msaidizi, Roina Reuben amesema Frank alikuwa na maendeleo mazuri ya masomo darasani.

“Maendeleo yake yako vizuri, kwa sasa ana wiki mbili tangu ahamishiwe hapa akitokea Shule ya Msingi Ivumwe jijini hapa,” amesema.