KOCHA wa Taifa Stars, Miguel Gamondi, ambaye alikuwa miongoni mwa watazamaji wa dabi ya Ligi Kuu Bara kati ya Azam na Yanga, amesema mchezo huo haukuwa na kiwango cha kuvutia.
Akizungumza baada ya mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Gamondi alisema soka kwake ni burudani na mashabiki wanatarajia kuona timu zikishambulia, kutengeneza nafasi na kufunga mabao, kitu ambacho hakikuonekana katika mechi hiyo.
“Unajua aina ya soka ninayopenda. Kwa mimi, siku zote soka ni burudani. Ni lazima timu zijaribu kufunga mabao na kutengeneza nafasi za kufunga. Leo hatukuona mambo hayo sana uwanjani,” alisema Gamondi.
Hata hivyo, alieleza kuwa hali hiyo inaweza kuchangiwa na uchovu wa wachezaji kutokana na ugumu wa ratiba ya michezo katika kipindi hiki cha msimu.
Gamondi aliongeza kwa kusema kuwa akilinganisha na dabi nyingine zilizowahi kuchezwa kati ya timu hizo, dabi ya safari hii haikuwa kwenye kiwango cha juu cha ushindani na burudani ambacho mashabiki wamezoea kuona.
Licha ya matokeo hayo, Yanga imeendelea kuongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara kwa kufikisha pointi 36, huku Azam FC ikishika nafasi ya pili ikiwa na pointi 28.
Kikosi cha Azam FC: Aishi Manula, Lusajo Mwaikenda, Pascal Msindo, Yoro Diaby, Yeison Fuentes, James Akaminko, Zidane Sereri, Himdi Mao, Feisal Salum, Iddi Selemani na Ashraf Kibeku.
Kikosi cha Yanga: Djigui Diarra, Israel Mwenda, Mohamed Hussein, Ibrahim Abdulla, Bakari Mwamnyeto, Mudathir Yahya, Maxi Nzengeli, Allan Okello, Laurindo Dilson, Prince Dube na Duke Abuya.