Januari Makamba Atoa futari kwa taasisi za dini Tanga.

Na Mashaka Mhando, TANGA

MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Januari Makamba, ametoa msaada wa futari kwa taasisi nane za kidini jijini Tanga, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono waumini katika mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Zoezi hilo lililofanyika Leo Machi 16 Jijini Tanga, limenufaisha taasisi za TAMTA, Maawal Chumbageni, Zahara Rashad, Shamsi Maarifa, Sururu, Noor-Hudaa, Abutwalib pamoja na Anisa.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, Makamba amesema hatua hiyo inalenga kuimarisha mshikamano, upendo na utamaduni wa kusaidiana, hususan kwa makundi yenye uhitaji katika kipindi hiki cha funga.

“Taasisi za dini zina nafasi kubwa katika kulea maadili mema kwa vijana na jamii kwa ujumla. Ni muhimu kuendelea kuzisaidia na kushirikiana nazo ili zijikite katika kutoa malezi bora,” amesema Makamba.

Kwa upande wao, viongozi na wanafunzi wa taasisi hizo wameishukuru hatua hiyo wakieleza kuwa msaada huo utasaidia kupunguza mahitaji ya chakula kwa wanafunzi na waumini wanaofanya ibada katika vituo hivyo.

Kwa mujibu wa mratibu wa msaada huo wa futari, Salimu Bawazir alisema, utoaji huo wa futari ni umekuwa sehemu ya utaratibu wa Makamba kushirikiana na jamii ya Tanga katika masuala ya kijamii na kidini ili kuchochea maendeleo na umoja mkoani hapa.

Bawazir alisema baada ya kupita na kugawa futari katika taasisi za dini, Jumatatu Machi 16 mhe Malamba ameandaa futari kwenye hoteli ya Kitalii ya Tanga Beach Resort kwa watu mbalimbali waliopewa mialiko maalum.