Morogoro. Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki, amewataka watumishi wa Wizara ya Maji pamoja na wadau wa sekta hiyo kuweka mpango madhubuti wa usawa katika upatikanaji wa huduma za maji kwa watu wenye mahitaji maalumu, wakiwemo wenye ulemavu.
Kairuki ametoa rai hiyo leo Machi 16, 2026 wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Maji inayoadhimishwa kitaifa mkoani Morogoro. Katika uzinduzi huo, wadau wa maji kutoka mikoa mbalimbali nchini, yakiwemo mashirika, asasi za kiraia na jumuiya za watumia maji, wameshiriki mdahalo wenye kaulimbiu ‘Maji na jinsia’ yenye lengo la kuleta usawa katika upatikanaji wa maji.
“Jukwaa hili ni fursa mahususi kuungana na Serikali katika kuangalia makundi maalumu, hasa wanawake wenye ulemavu na wanawake ambao wanalea kaya za wenye ulemavu.
“Kama mwanamke wa kawaida asiyekuwa na ulemavu anapata tabu kupata huduma ya maji, hebu mfikirieni huyu mwanamke mwenye ulemavu au anayekaa na watoto wenye ulemavu anapata taabu kiasi gani?” amehoji Kairuki.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mwajuma Waziri, amesema wizara imejipanga vizuri kuhakikisha maoni yanayotolewa na wadau katika mdahalo huo yanapokelewa na kufanyiwa kazi kadri itakavyowekekana.
Wadau wa maji kutoka taasisi mbalimbali za umma, binafsi pamoja na jumuiya za watumia maji wakifuatilia majadiliano kwenye mdahalo wa uzinduzi wa wiki ya maji ambayo kitaifa inafanyika mkoani Morogoro. Picha Hamida Shariff
Amesema mdahalo huo umeandaliwa maalumu kwa ajili ya kuwaweka pamoja wadau wa sekta ya maji, ili kujadili nafasi ya jinsia katika upatikanaji wa maji safi, usafi wa mazingira, pamoja na uhifadhi, usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji.
“Pia mdahalo huu unatumika kama jukwaa la kujadili mikakati ya kuboresha sera, mipango na ushirikiano wa wadau kuhakikisha huduma za maji zinapatikana kwa usawa na kwa uendelevu wa jamii yote,” amesema katibu mkuu huyo.
Naye mwakilishi wa mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la WaterAid, Christina Mhando, amesema shirika hilo linaamini maji si tu huduma, bali ni njia ya kufungua milango ya usawa wa kijinsia katika jamii.
Aidha, amesema jamii zinazopata huduma bora ya maji, hasa wanawake na wasichana, maisha yao hubadilika na wanapata afya bora, muda na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya kiuchumi, kijamii na hata masoko shuleni.
“Tumekuwa tunaweka kipaumbele cha usawa wa kijinsia katika miradi tunayotekeleza, ikiwemo ya maji, kwa kutambua kwamba uwekezaji katika huduma za maji si tu suluhisho la kiufundi bali ni kichocheo cha haki, heshima na mabadiliko ya kitabia,” amesema Mhando.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mussa Kilakala, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, amesema Serikali imewekeza fedha nyingi kwenye miradi ya maji kwenye wilaya hiyo na mkoa kwa ujumla, huku lengo likiwa kuhakikisha jamii inapata huduma hiyo kwa utoshelezi na uendelevu.
Ametaja mradi mmoja kuwa ni ujenzi wa Bwawa la Kidunda, lililopo Wilaya ya Morogoro, ambalo litasaidia kutatua changamoto ya maji katika mkoa wa Pwani na Dar es Salaam, na pia litasaidia kwenye shughuli za kilimo cha umwagiliaji.
“Pamoja na kwamba bwawa hili litaondoa changamoto ya maji mkoa wa Pwani na Dar es Salaam, Rais Samia Suluhu Hassan ameshaelekeza kuwa vijiji vya jirani vinavyozunguka bwawa hili lazima vinufaike na huduma ya maji,” amesema Kilakala.