*****
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa majengo ya kisasa ya Chuo cha Usafiri wa Anga (CATC) kinachojengwa katika eneo la Banana, Ukonga jijini Dar es Salaam, na kuipongeza Serikali kwa juhudi zake za kuimarisha miundombinu ya mafunzo ya sekta ya usafiri wa anga nchini.
Pongezi hizo zimetolewa leo Machi 16, 2026 na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Selemani Kakoso, wakati wa ziara ya kikazi ya kamati hiyo katika Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) kwa lengo la kukagua maendeleo ya ujenzi wa majengo mapya ya chuo hicho.
Kakoso alisema kamati hiyo imeridhishwa na hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa mradi huo na kubainisha kuwa ujenzi wa miundombinu mipya utaendana na hadhi ya mafunzo ya kimataifa yanayotolewa chuoni hapo.
Amesema kwa sasa miundombinu iliyopo chuoni hapo haikidhi kikamilifu mahitaji ya mafunzo ya kisasa ya usafiri wa anga, hivyo ujenzi wa majengo mapya utasaidia kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.
“Kamati imeridhishwa na jitihada zinazofanywa na Serikali katika utekelezaji wa mradi huu. Hata hivyo, tunaielekeza Serikali kuendelea kumsimamia mkandarasi ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na kwa ubora uliokusudiwa,” alisema Kakoso.
Aidha, aliishauri Serikali kuhakikisha mkandarasi analipwa kwa wakati ili kuepusha ucheleweshaji wa mradi huo pamoja na kusimamia usalama na masilahi ya wafanyakazi wanaotekeleza ujenzi huo.
Awali, Waziri wa Uchukuzi, Makame Mbarawa, alisema Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuwekeza katika sekta ya usafiri wa anga kupitia ujenzi, ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya anga pamoja na kuimarisha mifumo ya usimamizi.
Amesema uwekezaji huo pia unaenda sambamba na kuimarisha rasilimali watu yenye ujuzi wa hali ya juu, ambayo ni muhimu katika kukuza na kulinda usalama wa sekta ya usafiri wa anga.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania, Salim Msangi, alisema Chuo cha Usafiri wa Anga Tanzania kina nafasi muhimu kimkakati kwani ni miongoni mwa vyuo tisa barani Afrika vinavyotambuliwa kutoa mafunzo ya usalama wa usafiri wa anga.
Alisema kukamilika kwa mradi huo kutaimarisha zaidi hadhi ya chuo hicho kuwa kitovu cha ubora wa mafunzo ya usalama wa anga barani Afrika na kuongeza mchango wa Tanzania katika ukuzaji wa utaalamu wa anga kimataifa.
“Mradi huu ni uwekezaji wa moja kwa moja katika usalama na maendeleo endelevu ya sekta ya usafiri wa anga nchini,” alisema Msangi.
%20%20(8).jpg)