Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imetembelewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kwa lengo la kukagua eneo la mradi wa ujenzi na kujionea maendeleo ya ujenzi wa Majengo ya Kisasa ya Chuo cha Usafiri wa Anga (CATC) yaliyopo Banana–Ukonga, jijini Dar es Salaam.
Ziara hiyo ya kikazi iliongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mhe. Selemani Kakoso, ambapo wajumbe wa Kamati walipata fursa ya kukagua hatua mbalimbali za utekelezaji wa mradi na kujionea hali ya maendeleo ya ujenzi unaoendelea.
Katika ziara hiyo, Kamati ilipongeza jitihada za TCAA katika kusimamia utekelezaji wa mradi huo na kuisisitiza Mamlaka kuendelea kumsimamia kikamilifu mkandarasi anayetekeleza ujenzi ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vilivyokubalika.
Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mbarawa, alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuwekeza katika sekta ya usafiri wa anga kupitia ujenzi, ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya anga pamoja na kuimarisha mifumo ya usimamizi, akibainisha kuwa rasilimali watu yenye ujuzi wa hali ya juu ni msingi wa ukuaji na usalama wa sekta hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya TCAA, Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Salim Msangi alibainisha kuwa CATC ina upekee wa kimkakati kwa kuwa ni miongoni mwa vyuo tisa barani Afrika vinavyotambuliwa katika kutoa mafunzo ya usalama wa usafiri wa anga, hali inayoliweka Taifa katika nafasi muhimu ya kikanda na kimataifa katika ukuzaji wa utaalamu wa anga.
“Mradi huu unaimarisha nafasi ya CATC kama kitovu cha ubora wa mafunzo ya usalama wa anga barani Afrika na ni uwekezaji wa moja kwa moja katika usalama na maendeleo endelevu ya sekta ya usafiri wa anga nchini,” alisema.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu wakitembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa ujenzi wa Chuo cha Usafiri wa Anga (CATC) unaendelea katika eneo la Banana, jijini Dar es Salaam.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Selemani Kakoso na Menejimenti ya TCAA ikiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Bw. Salim Msangi wakisiliza maelezo kuhusu ujenzi wa mradi wa Chuo cha Usafiri wa Anga (CATC) yaliyokuwa yanatolewa na Meneja mradi wa Chuo cha CATC, Mhandisi Stephen Mwakasasa.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Selemani Kakoso akizungumza mara baada ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa ujenzi wa Chuo cha Usafiri wa Anga (CATC) unaendelea katika eneo la Banana, jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa akizumgumza kuhusu namna wizara inavyosimamia mradi wa Ujenzi wa Chuo cha Usafiri wa Anga (CATC) kinachojengwa katika eneo la Banana, jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) Salim Msangi akizungumza kuhusu maendelea ya mradi wa Ujenzi wa Chuo cha Usafiri wa Anga (CATC) kinachojengwa katika eneo la Banana, jijini Dar es Salaam.Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu pamoja na watumishi wa TCAA wakiwa kwenye kikao mara baada ya kamati hiyo kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa ujenzi wa Chuo cha Usafiri wa Anga (CATC) unaendelea katika eneo la Banana, jijini Dar es Salaam.
Ujenzi ukiendelea













