KATORO YAPOKEA GARI LA TANESCO KURAHISISHA USAMBAZAJI WA NGUZO.

Mapinduzi ya nishati ya umeme katika Jimbo la Katoro yameingia hatua mpya leo, baada ya kupokelewa kwa gari maalum la Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) lenye uwezo wa kubeba tani saba (7), likilenga kurahisisha usambazaji wa huduma.

Gari hilo limekuja wakati muafaka ambapo TANESCO imeanza kutumia nguzo za zege ambazo ni imara zaidi lakini zina uzito mkubwa ukilinganishwa na nguzo za miti zilizokuwa zikibebwa na watu hapo awali.

Kaimu Meneja wa TANESCO Mkoa wa Geita, Mhandisi Michael Mbwana, amebainisha kuwa gari hilo ni ukombozi katika ubebaji wa nguzo hizo nzito na litaongeza ufanisi wa kazi maeneo ya vijijini na mjini.

Akizungumza na wananchi waliojitokeza kulipokea gari hilo, Mbunge wa Jimbo la Katoro, Mhandisi Kija Limbu Ntemi, ametoa habari njema kuwa vitongoji 64 vilivyosalia sasa vitafikiwa na umeme kwa kasi zaidi.

“Gari hili litaongeza kasi ya usambazaji wa umeme. Nawaomba wananchi tushirikiane ili kwa pamoja tuijenge Katoro Mpya yenye nishati ya uhakika,” alisema Mhandisi Kija.

Kufuatia kukua kwa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Katoro na ongezeko la mahitaji ya umeme, Shirika hilo limeipandisha hadhi Katoro na kuifanya kuwa Wilaya ya Ki-TANESCO. 

Hatua hii inalenga kusogeza huduma za kiufundi na kiutawala karibu zaidi na wananchi ili kumaliza kero za kukatika kwa umeme na ucheleweshaji wa maunganisho mapya.

 Mbunge wa Jimbo la Geita Vijijini, Mhe. Joseph Kasheku (Msukuma), aliyekuwepo eneo hilo, amesema kasi ya ukuaji wa Katoro inatosha kuifanya kuwa Halmashauri inayojitegemea.

Mhe. Msukuma amemshauri Mhandisi Kija kupambana kuhakikisha Katoro inapata hadhi ya Halmashauri ili kuwapunguzia wananchi adha ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za kiserikali na kuchochea maendeleo ya mji huo wa kibiashara.

Nao wananchi wa Katoro wameonyesha kufurahishwa na hatua hiyo, wakisema kuwa kuwasili kwa vitendea kazi hivyo na kupanda hadhi kwa ofisi za TANESCO ni ishara ya wazi kuwa Katoro inakwenda kuwa kitovu kikubwa cha uchumi mkoani Geita.